TANGAZO


Wednesday, January 15, 2014

EPZA yavuka malengo 2013

*Yaimarisha uwekezaji Tanzania
 
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Dk. Adelhelm Meru (kushoto), akiwaongoza wafanyakazi na wageni waalikwa kulisakata Rhumba kwenye hafla ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014 kwenye Hotel ya Land Mark jana jijini Dar es Salaam. 
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) na wageni waalikwa wakilisakata Rhumba kwenye hafla ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014 kwenye Hotel ya Land Mark jana jijini Dar es Salaam.
Wageni waalikwa wakichukua chakula wakati wa hafla iliyoyoadaliwa na Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014 kwenye Hotel ya Land Mark jana jijini Dar es Salaam.  
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Dk. Adelhelm Meru, akimkabidhi zawadi maalumu mfanyakazi wa muda mrefu na mwenye umri mkumbwa wa mamlaka hiyo, Bi. Easter Mkumbwa (kulia) kwenye hafla ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014 kwenye Hotel ya Land Mark hivi karibuni jijini Dar es Salaam. (Picha zote na mpigapicha wetu)

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
KATIKA kile kinachoonyesha kuzidi kufanikiwa kwa Tanzania katika nyanja ya uwekezaji, Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) imetangaza kuvuka malengo yake kwa mwaka 2013.
Mafanikio hayo yalitangazwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Adelhelm Meru katika sherehe ya wafanyakazi ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha 2014 jijini Dar es Salaam.
“Pamoja na changamoto zilizopo hususani umeme, tunafurahi kuwa EPZA tumefanikiwa na kuvuka malengo tuliyokuwa tumejiwekea mwaka 2013,” alisema Dkt. Meru akiongea na waandishi wa habari.
Akiongelea baadhi ya vigezo walivyotumia kujipima katika mafanikio hayo, Dkt. Meru alisema mamlaka hiyo ilikuwa imejiwekea lengo la kupata wawekezaji wakubwa 25 lakini kufikia mwishoni mwa mwaka jana walikuwa wamepata wawekezaji 31 na hivyo kuvuka matarajio.
Pia alisema pamoja na kujiwekea malengo ya kuvutia mtaji wa Dola za Marekani 300 milioni kwa mwaka jana, mamlaka hiyo iliweza kuvuka lengo na kuingiza nchini mtaji wa jumla ya dola za Marekani 498 milioni nchini, ikiwa ni thamani ya fedha za wawekezaji walioingia nchini kwa mwaka huo.
Mkurugenzi huyo alisema EPZA ilikuwa imejiwekea lengo la kuzalisha ajira 5,200 kwa mwaka jana lakini hadi kufikia mwezi Disemba jumla ya ajira 10,200 zilikuwa zimezalishwa kutokana na uwekezaji mpya uliofanywa kupitia mamlaka hiyo.
“Tumevuka lengo hili kwa mara mbili na hii inatupa sana faraja kuwa kazi inafanyika,” alisema.
Akifafanua zaidi alisema EPZA ilikuwa imejiwekea lengo la kuuza nje bidhaa zenye thamani ya dola milioni 100 lakini lengo lilivukwa na kufikia dola milioni 1005.
Alisema mafanikio hayo yote ni matokeo ya kufanya kazi kwa bidii na kuwashukuru wafanyakazi wote wa EPZA kwa juhudi hizo.
“Napenda kuwashukuru sana wafanyakazi wote wa mamlaka hii kwa mafanikio haya,” alisema.
Aliishukuru serikali kwa msaada mkubwa inaoipa mamlaka hiyo katika kufanikisha malengo yake hasa katika kupata wawekezaji na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na kuweka miundombinu muhimu inayotakiwa katika maeneo hayo.
Alisema malengo ya mamlaka hiyo kwa mwaka 2014 ni kuvutia zaidi wawekezaji katika maeneo maalum ya uwekezaji hapa nchini na hivyo kuendelea kuimarisha uchumi wa nchi na kufikia maendeleo endelevu.

No comments:

Post a Comment