Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo hatimaye imesaini mkataba wa amani na waasi wa kundi la M23 waliokuwa wakifanya mashambulio ya mara kwa mara mashariki mwa nchi hiyo.
Waasi wa M23 walijilsalimisha mwezi uliopita baada ya kushindwa katika oparesheni iliyoendeshwa na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikisaidiwa na majeshi ya Umoja wa Mataifa. Alhamisi, marais Yuweri Museveni, ambaye ndiye mwenyekiti wa kongamano la kimataifa juu ya usalama katika maziwa makuu, na Joyce Banda, rais wa Malawi, ambaye ndiye mwenyekiti wa jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC, walisaini kama wadhamini wa mkataba huo.
Marais hao walisaini mkataba huo wakiwa jijini Nairobi walikohudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Kenya.
Juhudi za awali kutafuta amani kati ya serikali ya DRC na waasi hao wa M23 zilishindikana. Licha ya kuandikwa mktaba huo, pande mbili zilikataa kusaini kutokana na kushindwa kukubaliana jina litakalopewa. Upande wa serikali ya DRC ulisisitiza kuwa hakuna mkataba wa amani na waasi, hasa baada ya kuwa wamewashinda vitani.
Tangu kupigwa na kufukuzwa kwa waasi hao kutoka mkoa wa Kivu ya kaskazini, waasi hao wa M23 wamekuwa wakijisalimisha kwa serikali ya Uganda na kuomba hifadhi. Serikali ya DRC imetaka warudishwe nchini humo ili wakabiliwe na mashtaka ya mauaji, ubakaji na uhalifu mwinigne wa kivita. Hata hivyo Uganda imekataa kuwakabidhi ikisema kuwa ni wakimbizi na inasubiri uamuzi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi,UNHCR.
Pia viongozi wa nchi hizo mbili wakiwemo waakilishi wa jeshi wanasubiriwa kukutana kuamua hatma ya waasi hao waliojisalimisha.
Hadi sasa amani imeanza kurejea katika maeneo yaliyokombolewa kutoka mikono ya waasi wa M23. Hata hivyo mwandishi wa BBC katika eneo hilo Lubunga Bya Ombe, anasema kuwa bado serikali hiyo ya DRC ina kibarua kigumu kukabili makundi mengine madogo ya waasi yaliyo kita kambi katika eneo hilo.
Wiki hii serikali ya DRC ikishirikiana na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa imetangaza oparesheni mpya dhidi ya Kundi la waasi la FDLR.
No comments:
Post a Comment