TANGAZO


Tuesday, December 3, 2013

Maadhimisho ya Siku ya Walemavu Duniani

*Serikali kuongeza bajeti ya walemavu
 
Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na wajasiriamali wenye ulemavu wakati alipotembelea mabanda yao katika maadhimisho ya Siku ya Walemavu Duniani, Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam leo.
Rais Jakaya Kikwete akikata utepe kuzindua alama mpya za barabarani  kwa watu wenye ulemavu zilizobuniwa na Mwenyekiti wa Usalama Barabarani kwa Watu wenye Ulemavu, Jutoram Kabatelle (wa pili kulia). Kushoto ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Lupi Masanywa na kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza.
Rais Jakaya Kikwete akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wa huduma kwa watu wenye ulemavu, Mwakilishi wa Taasisi ya CCBRT, Meneja Utetezi, Fredrick Msigallah.
Rais Jakaya Kikwete akimshukuru Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu Wenye ulemavu Tanzania (Shivyawata), Lupi Masanywa, baada ya kumpatia tuzo maalumu kutokana na Serikali kuyapa kipaumbele masuala ya watu wenye ulemavu.
Mwenyekiti wa Usalama Barabarani kwa Watu wenye Ulemavu, Jutoram Kabatelle (aliyekaa), akiwapatia baadhi ya watu wenye ulemavu alama mpya za barabarani baada ya kuzinduliwa na Rais Jakaya Kikwete. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)


Na Charity James
SERIKALI imeahidi kutatua changamoto na kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu kwa kuanza na kuongeza bajeti katika mfuko wa walemavu.

Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam leo na Rais Jakaya Kikwete, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani.

Alisema lengo la maadhimisho hayo ni kukumbushana haja ya kuendelea kuchukua hatua za kuwahudumia na kuwaendeleza watu wenye ulemavu duniani.
''Watu wenye ulemavu wanayo haki ya kushiriki kupata mahitaji yao kama raia wengine wanavyopata haki zao, bila ya kubaguliwa,'' alisema.
Rais Kikwete aliwataka walemavu kuhakikisha wanachangamkia fursa ya elimu ili iweze kuwaweka katika hali nzuri na imara katika maisha bila kusubiri kuwezeshwa.
Alisema serikali itahakikisha inaendelea kuongeza fursa ya elimu kwa walemavu kwa kufufua vyuo na kuhakikisha inajenga vyuo vingine.
Miongoni mwa changamoto zilizotajwa na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Duniani (Shivyawata), Amon Anasaz, ni kukosekana kwa uwakilishi wa watu katika vyombo vingi vya maamuzi kuanzia ngazi za serikali za mitaa hadi serikali kuu.
Kukosekana kwa alama maalumu za barabarani ambazo zingewawezesha madereva na watu wengine kuziheshimu ili watu wenye ulemavu waweze kumudu kutumia barabara kwa uhuru.
Pia, kukosekana kwa miundombinu isiyo rafiki kwa watu wenye ulemavu, viziwi wamekuwa wakikosa taarifa muhimu zinazotangazwa kupitia luninga kutokana na kutokuwepo wakalimani wa lugha ya alama.

No comments:

Post a Comment