TANGAZO


Thursday, December 19, 2013

Mama Salma Kikwete apata Tuzo ya Uongozi uliotukuka nchini Dubai

 
Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake  na Maendeleo, WAMA, Mama Salma Kikwete  (akipokea tuzo ya Uongozi Uliotukuka kimataifa (Global Inspirational Leadership Award 2013) kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Maendeleo ya  Kiuchumi na Uongozi, Furo Giami, mwishoni mwa mkutano wa siku tatu wa Wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia.  Mkutano huo ulioandaliwa na Kituo cha Maendeleo ya Kiuchumi na Uongozi  (CELD), wakishirikiana na CEO Clubs Network na African Leadership Magazine uliofanyika Duba, Falme za Kiarabu (UAE).
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akitoa hotuba ya kushukuru mara tu baada ya kupokea tuzo hiyo huko Dubai
Wake wa marais kutoka Barani Afrika waliotunukiwa tuzo na Kituo cha Maendeleo ya Kiuchumi na Uongozi wakionesha tuzo, nishani na hati walizokabidhiwa kwa washiriki wa mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe na washiriki waliofuatana na msafara wa Mama Salma Kikwete kwenye mkutano wa wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia wakisherehekea na kumpongeza Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA, wakiongozwa na  Balozi wa Tanzania kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu, Mbarouk Mbarouk, mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo.

Na Anna Nkinda – Maelezo, Dubai
19/12/2013 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya kimataifa ya Uongozi wenye Hamasa kwa mwaka 2013 (Global Inspirational Leadership Award 2013) kutokana na  kazi anazozifanya za kuwasaidia wanawake na watoto wa kike nchini ambazo zimewahamasisha watu mbalimbali Duniani kuweza kuzisaidia jamii zenye mahitaji.

Hafla ya kukabidhi tuzo hizo ambazo zilitolewa jana  na Kituo cha  Maendeleo ya kiuchumi na Uongozi (CELD) cha nchini Nigeria zilifanyika katika Hoteli ya Atlantis, The Palm  iliyopo Dubai , Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Akiongea mara baada ya kukabidhiwa tuzo hizo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwashukuru waandaaji wa tuzo hizo  kwa kuona na kutambua umuhimu wa kazi anazozifanya na kukipongeza  kituo hicho kwa kazi wanayoifanya ya kuinua uchumi wa wanawake.

Mama Kikwete alisema vifo vingi vya wanawake vinatokana na uzazi, majeraha yanayosababishwa na ukeketwaji, ukatili wa kijinsia  vinaleta wasiwasi na changamoto za kibinadamu hivyo basi ni lazima wanawake wafanikiwe kukabiliana na hali hii kwa kuwa wengi wanakufa kutokana na sababu zinazoweza  kuzuilika pia wanakosa nafasi ya kujikwamua kiuchumi.

“Hatuna muda wa kupoteza lazima tuchukuwe hatua sasa bila ya kurudi nyuma kwa sababu zisizoeleweka nia ni kuweka nafasi yetu ya  uongozi wa kimataifa ambao utakuwa ni mfano wa kujivunia kwa wanawake huku tukiona  kuzaliwa kwa watoto kuwe ni hali ya kufurahia na siyo kipindi cha huzuni na kuomboleza”, alisema Mama Kikwete.

Alimalizia kwa kusema tatizo la vifo vya uzazi litaisha pale ambapo juhudi za makusudi zitafanyika, kuinua  hali ya maisha ya wanawake wa Afrika na nchi zinazoendelea jambo linalotakiwa ni kutambua kuwa Dunia ina rasilimali za kutosha, utaalamu na ujuzi wa kuweza kufanya mambo hayo.

Kwa upande wake  Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha   CELD Mama Furo Giami aliwapongeza wanawake hao viongozi kwa tuzo walizopewa na kusema hivi sasa wanawake wameweza kufanya njia kwa kuthubutu kupita njia ambayo wanaume walipita hapo zamani na  kufanya kazi nzuri zaidi ambayo imewaletea maendeleo.

Mama Giami alisema wanawake wengi wenye  sauti ndogo wameweza kuzitumia sauti zao kusikika katika jamii na  kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha yao. Wameweza kujitegemea na hivyo kupambana  na hali ngumu ya uchumi.

Kituo hicho ambacho kilitoa tuzo kwa wanawake  viongozi 15 kutoka nchi za Afrika, Asia na Mashariki ya kati kinafanya kazi za kuwainua wanawake na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuhakikisha kuwa wanatimiza malengo yao.

Wengine waliopewa tuzo hiyo ni pamoja na Mke wa Rais wa Namibia Mama Penehufipo Pohamba, Mke wa Rais wa Burundi Mama Dk. Mchungaji Denise Nkurunziza na Mke wa waziri Mkuu wa Malaysia Mama Datin Paduka Seri Rosmah Monsor.

Utoaji wa tuzo hizo ulifanyika mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku tatu wa wanawake kutoka nchi za Afrika, Asia na  Mashariki ya Kati ambao ulihudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa 28 na kujadili kuhusu Uongozi ni Elimu: Ufunguo wa mustakabali wa wanawake katika nchi zenye uchumi unaoibuka.

No comments:

Post a Comment