TANGAZO


Sunday, December 8, 2013

Dunia yazidi kumkumbuka Mandela

 


Nelson Mandela Rais wa ANC1962, kabla ya kifungo
 

Mwaka 1962 Nelson Mandela kwa siri na bila ruhusa aliondoka nchini Afrika Kusini na kutumia miezi saba akisafiri katika nchi mbalimbali barani Afrika.Chama cha African National Congress, ambacho kilipigwa marufuku na serikali ya ubaguzi wa rangi nchini humo, kilikuwa ndio tu kimeanzisha tawi lake la kijeshi lililojulikana kwa jina la Umkhonto we Sizwe.
 
Ziara hiyo ya Mandela ilikuwa ni kupata kuungwa mkono kisiasa na kifedha kutoka nchi za bara la Afrika, na kutafuta nchi ambazo zitakuwa tayari kutoa mafunzo kwa wapiganaji wake wanaojiunga na jeshi hilo, ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe. Alipata mafunzo ya kijeshi nchini Morocco kutoka kwa askari wa Algeria, waliokuwa wakitumia ardhi ya Morocco kama kituo cha kupambana na utawala wa kikoloni wa Ufaransa.

 
Na mafunzo mengi yalifanyika nchini Ethiopia. Fekadu Wakene ni kanali mstaafu wa jeshi nchini Ethiopia ambaye alipewa jukumu la kutoa mafunzo ya mbinu za kivita kwa Nelson Mandela.
Kanali Wakene anasema wakati huo hawakujua namna alivyofika hapo na sababu ya kuja kwake.

"Lakini tulipata maelekezo kutoka kwa viongozi wetu. Mkuu wangu wa kazi alikuwa Jenerali Tadesse Birru. Aliniita na kunitambulisha kwa mgeni na nilimpatia mafunzo.

Tulifanya mafunzo katika mambo mbalimbali kama vile kuhujumu miundo mbinu na kutega milipuko. Nmana ya kushambulia na namna ya kujificha au kuendesha mambo chini kwa chini. Na namna ya kuteketeza kundi la adui.

Tulikuwa tukifanya mafunzo ya nadharia mchana na usiku tulifanya mazoezi kwa vitendo."

Kanali huyo, anamwelezea Mandela kuwa alikuwa mwanafunzi imara sana na msikivu. Alifuata mafunzo vizuri na alikuwa ni mtu mwenye mvuto wa kupendwa. Huwezi kujizuia, bali kumpenda.

Anasema nje ya kazi alikuwa mwenye furaha, mtu mcheshi na wakati wa kazi alizingatia kile alichokuwa akikifanya kwa wakati huo.

Mandela alikuwa jasiri na msikivu.

"Kimwili alikuwa mtu mwenye nguvu sana na aliyejengeka. Lakini, wakati mwingine wa mafunzo, alikuwa mbele ya kile kilichofundishwa. Japokuwa nia yake ilikuwa nzuri lakini kilichokuwa kikifanyika kilikuwa cha hatari. Wakati mwingine tulimzuia kidogo kwa sababu za kiusalama.

Kanali Wakene anasema hawakufahamu mpaka baadaye kabisa waliposikia kuhusu Rais Nelson Mandela na habari yake.

"Nakumbuka kusikia kuhusu kuachiliwa kwake kutoka gerezani. Wakati huo ulikuwa wa furaha kubwa. Kila mahali mjini Addis, kila mtu alishangazwa na kufurahi habari zilipoeenea za kuachiliwa kwake."
Kwa upande mwingine kiongozi mpigania uhuru katika nchi jirani ya Zimbabwe, Rais Robert Mugabe naye anaeleza jinsi alivyomfahamu Nelson Mandela.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amemwelezea marehemu Nelson Mandela kama kinara wa wanyonge na dhamira yake ya ukombozi itaendelea kuenziwa nchini Zimbabwe.



Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe
Katika ujumbe wake wa rambirambi kufuatia kifo cha rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, rais huyo wa Zimbabwe amemwelezea Mandela kama mpigania haki.

Mandela amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95 nyumbani kwake mjini Johannesburg baada ya kuugua kwa muda mrefu akisumbuliwa na maambuzi katika mapafu na atazikwa tarehe 15 Desemba 2013.
Rais Mugabe jana alimtumia rambirambi rais Jacob Zuma akisema, "kwa niaba ya serikali na wananchi wa Jamhuri ya Zimbabwe na chama tawala cha Zanu-PF na mimi mwenyewe, ningependa kuelezea masikitiko makubwa kutokana na kifo cha mhimili mkuu wa ukombozi wa Afrika, mpigania uhuru na rais wa kwanza wa Afrika Kusini huru na ya kidemokrasia, Bwana Nelson Rolihlahla Mandela kilichotokea Desemba 5,2013.

Maisha ya kisiasa ya Bwana Nelson Mandela, ni kielelezo cha kutukuta na kitabakia kuwa nguzo ya uadilifu. Sio tu alikuwa kinara wa harakati za ukombozi wa mtu mnyonge bali pia alikuwa mnyenyekevu na kiongozi ambaye hakuonyesha ubinafsi katika kuwatumikia watu wake. Bwana Mugabe anasema wanaungana na taifa zima kuomboleza kifo cha Bwana Mandela.

Marehemu Nelson Mandela daima atabakia katika akili zetu kuwa mpigania haki.

No comments:

Post a Comment