Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Aron Msigwa – MAELEZO)
Na Aron Msigwa – MAELEZO.
SERIKALI imewataka wananchi kuzitumia ipasavyo fursa za Elimu zinazotolewa kupitia programu mbalimbali, ikiwemo Elimu ya Watu Wazima (EWW) na ile ya Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (ENMRA), ili kupunguza tatizo la umasikini, maradhi na ujinga.
Kauli hiyo imetolewa leo, jijini Dar
es Salaam na Mkuu wa Mkoa wa huo, Said Meck Sadiki wakati akitoa
taarifa kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya
Elimu ya Watu Wazima na Elimu ya Nje ya Mfumo Rasmi yatakayofanyika jijini Dar es
Salaam kuanzia Novemba 13, 2013, yakiongozwa na kauli mbiu “Kisomo kwa ajili ya
Karne ya 21”
Amesema serikali imeanzisha programu
mbalimbali za elimu kuanzia msingi mpaka sekondari kwa lengo la kuwawezesha
wananchi kupata fursa hiyo na kuondokana na tatizo Umaskini, maradhi na ujinga
na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi, Kijamii, Kisiasa na
Kiutamaduni.
Ameeleza kuwa mkoa wa Dar es salaam
kwa sasa unaratibu program mbalimbali zikiwemo Mpango wa Elimu ya Msingi kwa
walioikosa (MEMKWA) unaowahusisha wanafunzi wenye umri kati ya miaka 9 hadi 18
ambao husoma katika mfumo wa makundi rika.
Amesema jumla ya wanafunzi 1,846
wamejiunga na program hiyo kwa mwaka 2013 wakihusiha wale wenye umri wa miaka 9
mpaka 13 na 14 mpaka 18.
Bw. Meck Sadiki ameeleza kuwa mkoa wa
Dar es salaam pia unasimamia Mpango wa Uwiano kati ya Elimu ya Watu Wazima na
Jamii (MUKEJA) unaohusu utoaji wa Elimu kupitia kisomo cha kujiendeleza na
kisomo chenye manufaa kinachowahusisha watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 18
wapatao 1,678 waliojiunga kwa mwaka 2013.
Ameongeza kuwa wanafunzi wapatao
2,309 wamejiunga na programu ya Elimu ya Sekondari Huria (PESH) ambayo
huendeshwa kwa wanafunzi ambao wamekosa sifa za kuchaguliwa kujiunga na shule za
sekondari kupitia chaguo la mfumo rasmi.
“Wanafunzi wanaosoma katika mpango wa
PESH serikali imewawekea utaratibu wa kusoma katika shule za msingi na sekondari
ambazo hazina utaratibu wa awamu mbili za kusoma, wao husoma jioni baada ya muda
wa kawaida wa masomo”
Aidha amezitaja programu nyingine za
elimu zinazowahusisha watu wazima na vijana kuwa ni pamoja na Elimu ya Masafa
na Ana kwa Ana (ODL) ambayo ina jumla ya wanafunzi 335 wanaoendelea na masomo na
Elimu Changamani (IPPE) ambayo inawahusisha vijana 112 waliomaliza elimu ya
msingi na kukosa nafasi ya kujiunga na sekondari ambao hujengewa uwezo katika
masomo ya maarifa, ufundi, afya, maktaba na mazingira.
Kuhusu maadhimisho ya mwaka huu Bw.
Mecki Sadiki ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine yatakuwa na mchango mkubwa
katika kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu kusikiliza, kusoma na kutoa maoni
ya upatikanaji wa katiba mpya nchini, kuongeza mwamko kwa jamii katika masuala
ya elimu, kutathmini utekelezaji wa azimio la ulimwengu kuhusu utoaji wa elimu
kwa wote na kutathmini mafanikio na mapungufu ya utekelezaji wa Elimu ya Watu
Wazima (EWW) na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (ENMRA).
No comments:
Post a Comment