Polisi nchini Tanzania wamesema shehena ya Pembe za Tembo
zilizokamatwa katika bandari ya Zanzibar ni sawa na Tembo mia tatu na watano,
zikiwa na thamani ya karibu shilingi bilioni nane, sawa na karibu dola milioni
tano za Kimarekani.
Pembe hizo zilikuwa zimefichwa kwenye kontena la urefu wa mita 40, tayari kwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Serikali ya Tanzania iko katika kampeni kamambe ya kupambana na ujangili ili kunusuru wanyama pori ambao wako hatari kutoweka kutoka na kushamiri kwa biashara ya meno ya tembo na vipusa vya faru.
Iliripotiwa kuwa wastani wa tembo 30 huuawa kila siku nchini Tanzania, hali iliyoilazimisha serikali kukabiliana na mtandao wa ujangili, ambao unatuhumiwa kuunganisha watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wawindaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wakubwa ndani na nje ya nchi.
Hivi karibuni raia watatu wa China walikamatwa nchini Tanzania kwa kukutwa na pembe 706 ya tembo, sawa na Tembo 353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini humo.
No comments:
Post a Comment