Karibu watu ishirini wameuawa katika shambulio la kujitoa
mhanga kwenye kituo cha polisi nchini Somalia.
Shambulio hilo limetokea katika mji wa Beledweyne karibu na mpaka na
Ethiopia. Mashuhuda wameiambia BBC kuwa gari lilipiga lango kuu la kuingia
kwenye jengo la polisi na kulipuka kabla ya watu wenye silaha kushuka na
kushambulia jengo hilo kwa risasi. Taarifa zinasema wengi waliofariki katika
shambulio hilo ni maafisa wa polisi.Wapiganaji wa kiislamu wa Al Shabaab wamekiri kuhusika na shambulio hilo. Mwezi uliopita wapiganaji hao wa Al Shabaab pia walikiri kuhusika na shambulio jingine ambapo watu 16 waliuawa katika hoteli moja maarufu mjini Mogadishu.
Maafisa wa polisi nchini Somalia wamesema mlipuko huo ulikuwa ni mkubwa na umesababisha majeruhi kadhaa.
"Mlipuko ulikuwa ni mkubwa na pia wapo majeruhi kadhaa, hata hivyo hali imedhibitiwa," amesema Kanali Abdulkadir Ali, kamanda wa polisi wa mji huo wakati akiongea na shirika la habari la AFP.
Kamanda wa kundi la Al Shabaab Mohamed Abu Suleiman ameliambia shirika la AFP kuwa makomandoo wa Al Shabaab ndio waliofanya shambulio hilo.
Naye Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amesema shambulilo hilo ni la kujimaliza na linaonyesha kutojali maisha.
"Kipau mbele changu cha kwanza ni kutuma salamu za rambi rambi kwa waathirika na familia zilizoguswa na tukio hilo la kipumbavu", alisema katika taarifa yake
"Nimesema ni shambulio la kipumbavu kwa sababu maadui zetu wanapaswa kuelewa kwamba mashambulizi hayatawasaidia kuendeleza harakati zao zaidi sana yanawapotosha"
Mwezi Septemba, kundi la Al Shabaab lilisema kuwa lilifanya shambulizi la kigaindi katika kituo cha biashara cha Westgate nchini Kenya ambapo watu wapatao 67 waliuawa.
No comments:
Post a Comment