TANGAZO


Thursday, October 24, 2013

Wanajeshi wa UN wauawa Mali

 





Wanajeshi wa UN walichukua usukani kutoka kwa wanajeshi wa Ufaransa waliopambana na wapiganaji wa kiiisilamu kaskazini mwa Mali
 

Wanajeshi wawili wa Kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, wameuawa na wengine sita kujeruhiwa vibaya katika shambulizi la kujitoa mhanga Kaskazini mwa Mali.
Raia wa kawaida pia walifariki kwenye shambulizi lengine la bomu wakati mshambuliaji alipoingiza gari lake lenye mabomu katika eneo la kukagua magari kabla ya kujilipua mwenyewe.

Mtoto mmoja aliuawa na mwengine kujeruhiwa kwa mujibu wa taarifa za shirika la habari la Reuters likinukuu maafisa wa serikali.
Umoja wa Mataifa una takriban wanajeshi 6,000 nchini Mali, walioko huko kupambana na wapiganaji wa kiisilamu.

Katibu mkuu wa umoja huo Ban Ki-moon alisema kuwa mashambulizi hayo hayataathiri kabisa lengo la UN kuunga mkono kurejeshwa kwa utulivu na usalama pamoja na amani nchini Mali.
Baraza la usalama la UN limelaani mashambulizi hayo kwa kauli nzito sana.
Ilielezea kusikitishwa pamoja na kuwatakia pole jamaa na marafiki za wanajeshi waliouawa pamoja na serikali ya Mali na Chad.

Baraza huilo limesema kuwa waliohusika lazima watachukuliwa hatua kali na imeitaka Mali kuchunguza mauaji hayo na kuwaadhibu waliohusika nayo.
Wizara ya ulinzi ilisema kuwa washambuliaji wanne walihusika na mashambulizi hayo na wote walifariki.
Mwakilishi wa UN nchini Mali, Bert Koenders, mapema mwezi huu alitoa wito wa kupelekwa kwa wanajeshi zaidi baada ya kuongezeka kwa visa vya mashambulizi ya mabomu na makombora.
Wanajeshi wa Ufaransa, walikomboa eneo la Kaskazini mwa Mali pamoja na miji mingine kutoka kwa wanamgambo baada ya kuanzisha operesheni dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu.
Jukumu la usalama hata hivyo walilikabidhi kwa Umoja wa Mataifa mwezi Julai.

No comments:

Post a Comment