Shirika la kimataifa Amnesty International,linasema kuwa
maafisa nchini Misri wanawazuilia mamia ya wakimbizi wa Syria katika mazingira
mabaya sana.
Wakimbizi hao wanatoroka vita vinavyoendelea Syria.Katika ripoti yake mpya, shirika hilo linasema kuwa idadi kubwa ya watoto wanazuiliwa wengi wakiwa hawana wazazi.
Kwa mujibu wa shirika hilo, baadhi ya wakimbizi wamezuiliwa katika vituo vya polisi ambako hali ni duni wengi wakiwa hawapati chakula wala matibabu kwa walio wagonjwa.
Linasema kuwa mjini Alexandria , mapacha wawili wenye mwaka mmoja walipatikana miongoni mwa wale waliozuiliwa.
Maafisa wa utawala bado hawajajibu tuhuma za shirika hilo.
Misri imekuwa ikikumbwa na vurugu za kisiasa tangu kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa Rais Hosni Mubarak mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment