TANGAZO


Sunday, October 13, 2013

Mwandishi Ufoo Saro apigwa risasi na mchumba wake


*Afanyiwa upasuaji wa kuondoa risasi mwilini, Muhimbili 

*Apelekwa wodi 12 Kibasila

Ufoo Saro akiwa amepumzika baada ya kufanyiwa upasuaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam leo na kisha kulazwa wodi 12, jengo la Kibasila. (Picha zote Khamisi Mussa)
Muuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), akimpeleka wodini mwandishi na mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro,  baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondolewa risasi kufuatia kushambuliwa kwa silaha ya moto nyumbani kwa mama yake Kibamba jijini Dar es Salaam leo na mtu aliyedaiwa kuwa mchumba wake ambaye pia alimuua mama mzazi wa Ufoo Saro na kisha kujimaliza mwenyewe kwa kujipiga risasi.
 Wapigapicha wa vyombo vya habari mbalimbali wakimpiga picha Ufoo Saro baada ya kuondolewa chumba cha upasuaji.
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakimsindikiza Ufoo Saro wakati akipelekwa wodini.

Na Mwandishi wetu, jijini Dar es Salaam
MTANGAZAJI wa ITV Ufoo Saro amejeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi na mchumba wake ambaye baada ya tukio hilo naye alijipiga risasi na kufariki dunia papo hapo.


Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (ACP), Camilius Wambura alisema tukio hilo limetokea alfajiri ya kuamkia leo.


Kamanda Wambura amedai kuwa mwanaume aliyetenda mauaji hayo ni mchumba wake, alikuwa anafanya kazi katika umoja wa mataifa ( UN ) huko sudani ila bado haijafahamika kitengo alichokuwa akifanyia kazi.


Wambura, alisema inasemekana kulikua na ugomvi kati ya wawili hao ambapo walishindwa kuelewana na ndipo walipoamua kwenda kwa mama mzazi wa Ufoo Saro (mama mkwe) ili awasuluhishe.


Alisema baada ya usuluhishi kuanza na kuonekana kuwa tatizo liko kwa mwanaume, mwanaume huyo alimshutumu mama mkwe wake kwamba amekuwa na mazoea ya kumtetea mwanawe na ndipo alipotoa bastola na kumpiga mama yake na Ufoo Saro risasi ya kichwa na kumuua papo hapo.


Alifafanua kuwa alipomuua mama huyo, mwanaume huyo alimpiga Ufoo Saro risasi mbili , moja ya tumboni na nyingine ya mguuni na kudhani kwamba amemuua kumbe amemjeruhi tu kisha kujipiga mwenyewe risasi ya kidevuni na kufariki dunia hapo hapo.


No comments:

Post a Comment