TANGAZO


Wednesday, October 9, 2013

Mazishi ya kitaifa kwa wahamiaji Lampedusa


Baadhi ya watu waliofariki Lampedusa
Serikali ya Utaliana itafanya mazishi ya kitaifa kwa mamia ya wahamiaji waliokufa maji baada ya boti walimokuwa wanasafiria kuzama katika bahari ya Meditarenia kisiwani Lampedusa wiki jana.
Waziri mkuu Enrico Letta alitoa taarifa hiyo wakati wa ziara yake kisiwani humo akiambatana na Rais wa tume ya Ulaya Jose Manuel Barroso.
Bwana Barroso aliahidi kutoa dola milioni 40 kama ufadhili kuwasaidia wakimbizi nchini Utaliana.
Viongozi hao wawili walizomewa walipowasili kisiwani Lampedusa wakiwaita wauaji na wenye kuleta aibu.
Angalau watu 274 wengi wao raia wa Eritrea na Somalia - walifariki baada ya boti walimokuwa wanasafiria kuzama umbali wa kilomita moja kutoka ufuoni mwa kisiwa cha Lampedusa.
Ilikuwa moja ya majanga mabaya zaidi kuwahi kukumba Utaliana ikihusisha wahamiaji wanaokwenda kutafuta maisha bora barani Ulaya.
Lampedusa ni eneo ambalo hupokea boti nyingi sana kama hizo na wenyeji wamekuwa wakilalamika kuwa maafisa Utaliana na katika Muungano wa Ulaya hawajajitahidi katika kutatua tatizo la maelfu ya wahamiaji kufika katika kisiwa hicho kila mwaka.
Bwana Barroso na Bwana Letta walitembelea kituo cha muda cha kuhifadhi maiti huku akishika majeneza ya walioangamia. Baadaye alikutana na waathiriwa walionusurika kifo pamoja na wale walioendesha shughuli ya uokozi.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Barroso alisema kuwa hatawahi kusahau picha ya mamia ya majeneza aliyoyaona.

No comments:

Post a Comment