Msemaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
jinsia na Watoto, Erasto Ching‘oro (kushoto), akizungumza na
waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam, kuhusu mafanikio waliyoyapata
tangu kuzinduliwa kwa Mtandao wa Mawasiliano ya Kuwasaidia Watoto
wanaofanyiwa Ukatili Na. 116 (Child Help Line), Idara ya Habari, Maelezo. Kulia
ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa. (Picha zote na Eliphace Marwa)
Msemaji wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia na Watoto, Erasto Ching‘oro (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam, kuhusu mafanikio waliyoyapata tangu kuzinduliwa kwa Mtandao wa Mawasiliano ya Kuwasaidia Watoto wanaofanyiwa Ukatili Na. 116 (Child Help Line), Idara ya Habari, Maelezo. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa.
Ndugu
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari, MAELEZO,
Ndugu
Wanahabari,
Mabibi
na Mabwana,
Awali
ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kukutana nanyi; napenda
pia kuwashukuru ninyi Wanahabari kwa kuweza kuhudhuria kikao hiki.
Mnamo tarehe 14 Juni, 2013, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya watoto ilizindua Mtandao wa
Mawasiliano ya Kuwasaidia Watoto wanaofanyiwa Ukatili Na. 116
(Child Help Line). Mtandao huu ulizinduliwa kutokana na kuwepo kwa matukio mengi
yaliyokithiri ambayo yamekuwa yakiwakabili watoto hapa nchini. Madhumuni ya
uzinduzi wa mtandao wa mawasiliano na 116 ni kuwezesha watoto na jamii kwa kuripoti
matukio ya ukatili wanaofanyiwa watoto ili kuwaunganisha na mamlaka husika kuhakikisha
kuwa mtoto anapata huduma na ulinzi stahiki.
Ukatili
huo ni pamoja na kubakwa, kuchomwa moto, kutelekezwa, unyanyasaji mbalimbali na
wakatai mwingine kuuawa. Ukatili huo kwa kiasi kikubwa umekuwa ukiathiri
maendeleo ya watoto, makuzi ya watoto pamoja na kuwasababishia madhara ya kisaikolojia.
Ndungu
Wanahabari,
Matokeo
ya Utafiti uliofanywa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
(2009) kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Afya
ya Sayansi na Tiba cha Muhimbili, UNICEF pamoja na Kituo cha Kudhibiti na
Kuzuia Magonjwa (CDC) ambao ulihusu kuelewa tatizo na sura ya ukatili wa
kijinsia, kimwili na kiakili wanaofanyiwa
watoto nao ulichangia kuona umuhimu wa kuwa na mtandao wa mawasiliano ili
kusaidia utoaji wa taarifa ya matukio ya ukatili na kuwaunganisha watoto na wasimamizi
wa ulinzi wa mtoto.
Kutokana
na ukweli kwamba, matokeo ya utafiti huu yalionyesha kuwa kuna kiwango kikubwa
cha ukatili dhidi ya watoto na matukio mengine ya ukatili dhidi ya watoto
yamekuwa yakifanyika ama shuleni, nyumbani na ndani ya jamii. Hali hii ilipelekea
wadau wa masuala ya watoto kuandaa
Mpango Mkakati wa mwaka mmoja wa Kushughulikia Tatizo la Ukatili Dhidi ya
Watoto (2012 – 2013); na hatimaye kuandaa Mpango wa Miaka Mitatu wa
kushughulikia tatizo hilo (2013 – 2016) ambao ulizinduliwa mkoani Dodoama mwezi
Aprili, 2013.
Ndugu
Wanahabari,
Pamoja
na jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba kunakuwepo na Sera ya Maendeleo ya Mtoto
(2008), Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009, uanzishaji wa Madawati ya Jinsia
na Watoto katika vituo mbalimbali vya polisi nchini; bado Wizara na wadau tuliona
kuna umuhimu wa kuwa na chombo kingine ambacho kitasaidia upatikanaji wa taarifa
za matukio ya ukatili kwa watoto ili kuwaunganisha watoto na taasisi zinazotoa huduma
ya stahiki kwa watoto walioathirika.
Mapema
tarehe 3 Januari, 2013 Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ilifikia
makubaliano na Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya C-sema kuhusu uendeshaji wa
mtandao wa mawasiliano ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto Na 116 ili kuripoti
matukio ya ukataili wanaofanyiwa na kuwasilisha taarifa hizo kwa watoa huduma.
Kwa kuanzia, Mtandao huu unafanya kazi katika Wilaya na Manispaa za Temeke, Magu, Bukoba
Vijijini, Musoma Mjini, Kasulu, Hai, Manispaa za Ilala na Kinondoni kama eneo
la majaribio.
Mafanikio;
Ndugu wanahabari,
Toka mtandao huu ulipozinduliwa ni
kipindi cha mwezi mmoja na takriban wiki tatu. Hata hivyo mtando umeonesha
mafanikio kwa kuwepo mwitikio mkubwa kwa wananchi katika kutoa taarifa za ukatili
kwa watoto na kuonesha umuhimu wa upatikanaji wa msaada wa kisheria na hivyo kuharakisha
jukumu la utoaji wa huduma kwa mtoto aliyefanyiwa ukatili katika maeneo
mbalimbali.
Tangu kuanzishwa Mtandao wa
Mwasiliano ya Msaada wa Kuzuia Ukatili wa Watoto mapema tarehe 12 Mei 2013
kumekuwepo na mafanikio makubwa. Kwa kipindi kinachoishia tarehe 18 Julai 2013
kiasi cha simu 1,146 zilipokelewa kutoka mikoa mbalimbali. Kati ya simu hizo, simu
235 zilihitaji
kufahamu jinsi mtandao unavyofanya kazi na namna ya kuripoti matukio ya
ukatili.
Simu 29
zilihitaji huduma ya ushauri na msaada zaidi ambapo taarifa za matukio ya ukatili
zilipelekwa kwa Kamati za Ulinzi na Usalama wa Mtoto katika ngazi ya Wilaya kwa
ajili ya ufuatiliji. Kamati hizi zinahusisha Maafisa Ustawi wa Jamii wa
halmashauri, Maafisa Maendeleo ya jamii, Polisi- Dawati la Jinsia na watoto.
Ndugu Wanahabari,
Takwimu hizi zinaonesha mafanikio
makubwa ya matumizi ya namba 116, kutokana na ukweli kwamba wakati wa uzinduzi
tarehe 14 Juni 2013 ilielezwa kuwa kulikuwa na jumla ya miito ya simu 267. Kati ya simu hizo,
simu 64 zilipokelewa wiki ya kwanza, wiki ya pili miito 96 na hadi siku ya
uzinduzi simu 107.
Hadi sasa kuna ongezeko la simu 939 kwa kipindi cha mwezi
mmoja. Idadi hii ya miito ya simu inaashiria kuwa kunamwitikio mkubwa kutoka
kwa wananchi katika kuripoti ukatili dhidi ya watoto katika maeneo tunakoishi. Vilevile,
taarifa hizi ni kielelezo cha kuwepo kwa matukio ya ukatili wanaofanyiwa watoto
katika familia na jamii kwa ujumla..
Hili linathibitishwa na baadhi ya kesi
ambazo zinaripotiwa na wananchi likiwemo tukio ambalo lilifanyika Mkoani Arusha
ambapo raia mwema kwa niaba ya mama mzazi wa mtoto alipiga simu akiripoti tukio
la ukatili aliofanyiwa mtoto wa kike (umri 12) ambaye alitekwa na bwana mmoja, alimbaka
mtoto huyo na kisha mbakaji akamshikilia binti huyo mwanafunzi wa darasa la
sita na kuendelea kuishi naye kama mke.
Ndugu wanahabari,
Kuwepo kwa mawasiliano ya msaada wa
simu Namba 116 kuliweza kusaidia kumwokoa mtoto huyo kwa ushirikiano kutoka Jeshi
la Polisi Arusha ambao waliweza kumrejesha mtoto huyo nyumbani na kuendelea na
masomo yake. Hivyo, Wizara inazidi kuwaomba ninyi wanahabari kuendelea kuelimisha
wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia huduma hii ili kwa pamoja tuweze kuzuia na kudhibiti
ukatili dhidi ya watoto. Juhudi hizi zikiunganishwa na jitihada za vyombo vya
habari na wadau wengine tutaendeleza azma ya kuwa na jamii inayowajali na
kuwalinda watoto.
Aidha ni matumaini ya Wizara kuwa
wadau mbalimbali wataendelea kujitokeza kushirikiana na Wizara na asasi ya C-Sema
katika kuhakikisha kuwa huduma hii ya mawasilino inapatikana katika maeneo yote
hapa nchini katika muda muafaka ili kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata
ulinzi wa kutosha, na kwamba kila mwananchi anawajibu wa kuwalinda watoto na
kuzuia vitendo vya ukatili.
Ndugu Wanahabari,
Wizara inaendelea kuhimiza jamii kubadilika
na kuhakikisha kuwa familia ambayo ndio kitovu cha jamii panakuwa ni mahala
salama penye upendo amani na mshikamano miongoni mwa wanafamilia; na kuwapatia
watoto haki zao za msingi ikiwemo haki ya kuishi, kulindwa, na kuendelezwa.
Jamii inapaswa kukumbuka kwamba Haki ya mtoto ya kuishi
ni haki yao ya Kikatiba, hivyo kumnyima mtoto haki hiyo ni kukinzana na Mkataba
wa Kimataifa wa Haki na Ustawi wa Mtoto, Sera ya Maendeleo ya Mtoto na Sheria
ya Mtoto Na. 21 (2009). Hivyo, jamii inawajibu wa kulinda na kutetea utu na
uhai wa mtoto, ili kuhakikisha kuwa watoto wanaishi kwa amani, furaha, uhuru na
utulivu.
Mwisho napenda kuwashukuru
wanahabari kwa kuendelea kufichua na kuripoti taarifa nyingi za ukatili
wanaofanyiwa watoto kutoka katika maeneo mbalimbali. Napenda kuwathibitishia
kuwa taarifa zenu zimekuwa kikifanyiwa kazi na mamlaka husika katika ngazi
mbalimbali ili kuwasaidia watoto wetu wanaokumbwa na ukatili. Kwa pamoja
tunaweza kumlinda mtoto wa Tanzania na kumwekea mazingira rafiki.
Asanteni kwa Kunisikiliza
ErastoT. Ching‘oro
Msemaji
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia na
Watoto



No comments:
Post a Comment