TANGAZO


Wednesday, August 14, 2013

Nyumba zilizojengwa katika makaburi ya Mtwivila zavunjwa rasmi

Mgambo  wa  Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa na  viongozi mbali mbali wakielekea  kuvunja nyumba zilizojengwa makaburi ya Mtwivila  leo

Mgambo  wa Manispaa ya  Iringa na mwanasheria  katikati Bw Innocent Kihaga  wakielekea  kuvunja nyumba  zilizojengwa makaburini Mtwivila

Mgambo  wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa  wakivunja  nyumba  iliyojengwa katikati ya makaburi ya Mtwivila
Kaburi  hili la Rashid M. Lukuvi likiwa  jirani kabisa na ukuta  wa nyumba  hiyo iliyovunjwa

Mgambo  wakivunja nyumba  iliyokuwa ikijengwa katika makaburi ya Mtwivila mjini Iringa  leo


Nyumba  iliyojengwa makaburini  yavunjwa  rasmi leo na mgambo wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa
Makaburi  yaliyozunguka  nyumba  hiyo
Hii  ndio  nyumba ambayo ipo  jirani na kaburi la marehemu Idd Chonanga aliyekuwa  diwani wa kata ya Nduli kaburi  lenye mashada kushoto ,na hapo  waliposimama mgambo ndipo alipokaa waziri mkuu Mizengo Pinda  wakati wa mazishi na viongozi mbali mbali  wa mkoa wa Iringa
Uvunjaji wa  nyumba ambayo nje katika msalaba hapo ndipo  waziri mkuu Mizengo Pinda alikaa wakati wa mazishi ya diwani Chonanga ,nyumba  hii imevunjwa  sehemu ya ukuta na mmiliki wake amepewa  siku 30  kuanzia  leo  kuivunja
Mgambo  wakivunja  nyumba  iliyojengwa  eneo la makaburi ya Mtwivila mjini Iringa
Wananchi ambao  wamezika  ndugu  zao katika makaburi hayo  wakishuhudia  zoezi hilo
HATIMAYE Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa imeivunja nyumba  iliyokuwa ikijengwa katikati ya makaburi  ya Mtwivila   ambayo  iliripotiwa na mtandao huu  na  vyombo mbali mbali  vya  habari likiwemo gazeti la Jamboleo , radio Ebony Fm na  radio Cloud FM  pamoja na   nyumba nyingine mbili ambazo pia zilikuwa  zikianzwa  kujengwa eneo hilo .

Pamoja na  kuendesha  zoezi la  kuzivunjwa  nyumba  hizo ambazo  zilikuwa katika  hatua ya mwanzo  kabisa  pia Halmashauri hiyo  imetoa  muda wa  siku  30  kuanzia  leo  kwa mmiliki  wa  nyumba nyingine iliyokutwa  imekamilika ambayo pia  imejengwa karibu na makaburi ya Mtwivila eneo ambalo waziri Mkuu Mizengo Pinda alikaa wakati  wa mazishi  ya  aliyekuwa diwani wa kata ya Nduli marehemu Iddi Chonanga

Hatua ya  kuvunjwa kwa makaburi hayo  imekuja  ikiwa ni  siku  mbili zimepita  baada ya mtandao huu  wa matukio daima  kuibua suala  hilo  kuibua ujenzi huo holela  na  ni  siku  moja  baada ya mkurugenzi mtendaji  wa halmashauri ya  Manispaa Bi  Terresia  Mahongo  kutoa agizo kwa  maofisa mipango  miji , afisa ardhi na mwanasheria  wa Manispaa ya  Iringa  kufika  eneo hilo  ili  kuchukua hatua sitahiki.

Zoezi la  kuvunja nyumba  hizo  leo  majira ya  saa 3 asubuhi limeongozwa na maofisa mbali mbali  wa Manispaa ya  Iringa akiwemo mwanasheria  wa Halmashauri  hiyo Bw Innocent Kihaga pamoja na mgambo  zaidi ya  watano wa Halmashauri  hiyo.

Kuvunjwa  kwa  nyumba  hizo  kumeshuhudiwa na umati  mkubwa wa  wananchi  wa  maeneo mbali mbali ya mji  wa Iringa ambao  walifika  kushuhudia  utekelezaji  wa agizo la mkurugenzi baada ya  baadhi  yao  kudai  wamiliki wa nyumba  hizo  wamejenga katika makaburi ya ndugu  zao  hivyo  walikuwa  wakishindwa  kuchukua hatua  kutokana na kutojua  wahusika  wa  ujenzi huo wa nyumba makaburini.

Miongoni mwa makaburi yaliyokuwa hatarini  kuvunjwa na  wajenzi  wa nyumba  hizo ni pamoja na kaburi la Rashind  M. Lukuvi ambalo lilikuwa hatarini  kuvamimiwa na  wajenzi hao  iwapo ujenzi  huo ungefumbiwa macho.

Wakipongeza  hatua  iliyochukuliwa na uongozi  wa Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa  wananchi  waliofika  eneo  hilo kushuhudia  zoezi akiwemo Yustina Malinga , Yohana  Sanga na Juma  Ally   walisema  kuwa  mbali ya  kupongeza  uongozi  wa Manispaa chini ya mkurugenzi  wake  Bi Mahongo kwa  kuchukua hatua  ila  bado  waliwataka  wananchi  wenzao  wanaoendelea  kujenga makaburini  kuwa na huruma na  marehemu  waliozikwa katika maeneo  hayo kwani watambue kuwa hata  hao marehemu  walikuwa kama  wao .

Alisema  Bi Malinga  kuwa  wakati mwingine  wananchi  wamekuwa  wakiitafua  ugomvi  serikali kwani kitendo  cha  kujenga katika makaburi  ni  kinyume na tamaduni za  kitanzania  na  kuwa makaburini  ni eneo la kuishi wafu  sasa mtu  mzima  na familia  yako kujenga makaburini   utajiweka katika mazingira  ya  kuogopwa na  kila mtu.

Huku kwa  upande wake mzee  Sanga  akisema  kuwa  mbali ya  wananchi hao  awali kuonekana  wakilima maeneo  hayo ila bado baada ya  kuona hakuna mtu anayewafuatilia  waliamua  kujenga  kabisa.

"Tunawaomba  hawa  ndugu ambao inasemekana  si  wenyeji wa  eneo  kutumia utu  kabla ya  kuanza  kuvamia makaburi  yetu na kuanza  kujenga nyumba juu ya makaburi ya ndugu  zetu.....pia  tunaomba wahusika  wasakwe ili  wachukuliwe hatua kali za kisheria"

Mbali ya  kutaka  wahusika  hao kusakwa  bado  walielekeza  lawama  zao kwa  watendaji wa mitaa na kata  kwa  kushindwa  kuwawajibisha  wananchi wanaojenga  kiholela katika milima na maeneo ya makaburi kama  hayo.

Mwanasheria  wa Manispaa ya  Iringa Bw Kihaga  alisema  kuwa  wamelazimika  kuvunja nyumba  hizo baada ya  kuonekana zimejengwa maeneo ambayo si rasmi na  bila kibali  cha mipango miji .

Hata  hivyo  mwanasheria  huyo  alisema  wametoa  muda wa  siku 30 kwa mmiliki wa nyumba iliyopo  jirani na makaburi eneo  ambalo  waziri mkuu Mizengo  Pinda alikaa wakati wa mazishi ya diwani Chonanga  kuivunja  nyumba  hiyo ndani ya  siku 30  kuanzia leo kabla ya  kuvunjiwa nyumba hiyo na  kufikishwa mahakamani.

Pia  alisema  kuanzia  sasa msako mkali kwa  wote  waliojenga maeneo ambayo si rasmi na  wale  wanaojenga  bila  vibali  litaanza katika mji mzima  wa Iringa na  kuwataka wananchi  wanaotaka  kujenga  kufuata  sheria  ya ujenzi ikiwa ni pamoja na kutafuta ardhi halali  na kabla  ya  kujenga ramani  zao kupitisha ili  kupewa  kibali  cha ujenzi zaidi ya hapo  watachukua hatu.

Awali  mkurugenzi  wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa Bi Mahongo  aliwataka  wananchi kuheshimu  sheria na kuwa  hatakubali  kuona  ujenzi  holela unaendelea katika maeneo mbali mbali ya mji  wa Iringa na  kuwataka  wananchi  kutoa ushirikiano kwa  kufichua  watu  wanaojenga nyumba  kiholela na  kuvamia maeneo  ya  wazi .

Hata  hivyo  kutokana na uchunguzi wa kina uliofanywa na mtandao huu  wa  www.matukiodaima.com umebaini  kuwepo maeneo mengi zaidi ambayo  wananchi  wamejenga  kiholela yakiwemo maeneo ya Mtwivila ,Mwang'ingo , Zizi la Ng'ombe, Ipogolo  na  Semtema ambako wananchi  wameamua  kujenga hadi katika vilele  vya  milima .

No comments:

Post a Comment