Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Temeke, Joyce
Msumba, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, wakati
alipokuwa akielezea utendaji kazi wa manispaa hiyo. Kulia ni Mhasibu, Kitengo
cha Mapato, Zacharia Mbedule na Katikati ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya
Habari, Zamaradi Kawawa.
Mchumi wa Manispaa ya Temeke, Edward Simon, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu suala la ukusanyaji mapato.
Mhasibu Kitengo cha Mapato, Zacharia Mbedule, akifafanua jambo kwa waandishi wakati wa mkutano huo wa kuelezea kuhusu ukusanyaji mapato kwa manispaa hiyo.
|
Utangulizi
Manispaa ya Temeke ni moja kati ya Halmashauri zinazounda Jiji la Dar-es-Salaam, nyingine ni Ilala na Kinondoni, ina eneo la kilometa za mraba 656 na ukanda wa pwani wa kilometa 70. Inapakana na bahari ya Hindi kwa upande wa Mashariki, kusini na Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Ilala kwa upande wa kaskazini na magharibi. Ki-utawala manispaa ya Temeke imegawanywa katika majimbo mawili yaTemeke na Kigamboni , tarafa 3 , kata 30 na Mitaa 180.
Kulingana
na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Manispaa ya Temeke ina jumla ya watu
1,368,881, wanaume 669,056 na wanawake 699,825. Wakazi hawa wanajishughulisha
na ajira rasmi viwandani na maofisi , kilimo na sekta isiyo rasmi.
Lengo
la Manispaa ya Temeke kuitisha mkutano huu,
ni ili iweze kushirikiana na
wanahabari kuuhabarisha umma, na hasa
wakazi wa Temeke juu ya ukusanyaji wa mapato na mafanikio tuliyofikia pia
changamoto zinazotukabili katika kutoa huduma kwa jamii.
Ukusanyaji Mapato
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke
inategemea mapato yake kutokana na vyanzo mbalimbali, ikiwemo vyanzo vya ndani,
ruzuku kutoka serikali kuu, michango ya wadau mbalimbali wa maendelo na wahisani , pamoja na nguvu za
wananchi, ikiwa ni kwa mujibu wa sheria
ya fedha ya serikali za mitaa (Local Government Finance Act Na. 8 ya mwaka
1982).
Mapato yake yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka
ambapo katika mwaka wa fedha 2011/2012 kumekuwa na ongezeko kubwa zaidi.
Sababu za ongezeko na mafanikioOngezeko la mapato limetokana baada ya kuanzishwa utaratibu wa kuwa na mameneja wa vyanzo vyote vikubwa na wao kusimamia kwa karibu zaidi. Makusanyo ya mapato ya ndani yameongezeka kutoka shilingi bilioni tatu milioni mia nane tisini na moja na ishirini na tano elfu mia tatu arobaini na sita (3,891,025,346.00) mwaka 2005/2006 hadi shilingi bilioni ishirini na tano, milioni mia moja sabini na tano, hamsini na tatu elfu na tisa (25,175,053,009.00) mwaka 2012/2013, ukusanyaji umefikia asilimia 112.2% ya mapato.
Kutoa elimu kwa walipa kodi, ada
na ushuru mbalimbali, na matumizi ya GIS (Geographical Information System) na
MRECOM (Municipal Revenue collection Manager), kwa ajili ya kukusanya na
kutunza takwimu za wanaolipa ushuru wa mabango (bill Boards), huduma za jiji (
Service levy), kodi ya Majengo (Property
tax), na nyumba za kulala wageni ( hotel levy) .
Pia kuwatambua walipa kodi wa
vyanzo mbalimbali ambao wanalipa kodi ama ushuru bila shuruti, kukaa nao pamoja
kujadiliana juu ya kuboresha ukusanyaji huo na kuwazawadia wanaofanya vizuri
katika kulipa kodi kwa hiyari; zoezi hilo linafanyika kila mwaka kuanzia mwaka
2011/2012 ambapo kuna siku rasmi ya mlipa kodi kila mwaka ambayo ni tarehe 10
Novemba.
Toka kipindi cha mwaka 2005 hadi
2012/2013 uboreshaji wa utoaji huduma muhimu umeongezeka kama miundombinu (barabara
za lami kutoka km 166-173km), ujenzi wa
masoko (3-15), shule za sekondari (5-39) na utoaji huduma za afya (zahanati 19-28), ujenzi huu umetokana na vyanzo vya
ndani.
Kuhusu uzoaji taka, mwaka 2005
kiasi cha taka kilicho zolewa na kupelekwa dampo ni tani 102,220 sawa na asilimia 39.5 ya
taka zilizozalishwa (tani 258,785). Mwaka 2012 kiasi cha taka zilizozolewa na
kupelekwa dampo ni tani 195,224 ambayo ni asilimia 47 ya tani 415,370
zilizozalishwa.
Changamoto
Kwa kuwa majukumu ya Serikali za
Mitaa ni kutoa huduma kwa wananchi,na
kwa kuwa huduma hizo zinahitaji rasilimali fedha,bado kuna changamoto kwa Wadau
wa maendeleo kushiriki kikamilifu kuunga mkono juhudi za Halmashauri yetu za kuwahudumia
wakazi wake katika kulipa kodi, ushuru na ada mbalimbali zilizowekwa kwa mujibu
wa sheria ili halmashauri iweze kutoa huduma bora kwa wakazi wake kwaajili ya
ustawi wa maendeleo yao.
Ongezeko la idadi ya watu; hasa wahamiaji
kutoka katikati ya jiji na kutoka mikoa
mingine kuhamia Manispaa ya Temeke katika mitaa ya Mbagala rangi tatu , Charambe, Kongowe,Tandika,
Makangarawe na maeneo mengine , hii huiongezea halmashauri mzigo wa utoaji
huduma.
Ongezeko la uchafuzi wa mazingira
unaosababishwa na utupaji ovyo takataka.
Kuchelewa kwa ruzuku kutoka Serikali kuu, na wahisani kunasababisha
mapungufu katika ukamilishaji wa baadhi ya miradi iliyopangwa kwa kipindi
husika.
Ujenzi holela wa makazi, kutokana na idadi kubwa ya wahamiaji
ambao wanataka kuishi maeneo ya mjini, uchache wa watendaji na vitendea kazi.
Ukusanyaji usiokidhi/kufikia malengo ya kodi ya majengo
inayokusanywa na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA)
Mikakati tuliyojiwekea
Kuhimiza wananchi na wadau wengine kuendelea kuchangia miradi
inayotekelezwa katika ngazi ya jamii,hususani ujenzi wa
sekondari,zahanati,barabara,visima vya maji nk.
Halmashauri itahakikisha ifikapo mwaka 2015 vyanzo vyote vya
mapato vinakusanywa kupitia mifumo ya kompyuta.
Ufuatiliaji wa karibu sana utaendelea kufanyika kwa vyanzo
vyote vya mapato ikiwemo Huduma za Jiji (service levy) leseni za biashara, Kodi
ya Majengo (Property tax),kodi ya mabango( Bill boards), na ushuru wa nyumba za
kulala wageni na nyinginezo kwani vyanzo
hivi vimeonyesha mafanikio makubwa sana kama vitafuatiliwa kwa karibu.
Halmashauri itaendelea na ushirikino wa karibu na TRA ili kuongeza makusanyo ya mapato ya kodi ya
majengo.
Na mwisho ni kuendelea kutoa elimu kwa walipa kodi kwa njia
mbalimbali ili waweze kutimiza wajibu wao bila shuruti na Halmashauri iweze kutoa
huduma bora.
No comments:
Post a Comment