TANGAZO


Wednesday, July 24, 2013

Wahamiaji wazama kisiwani Java




Serikali ya Australia imebadili sera ya uhamiaji hasa kwa wale wanaoingia nchini humo kwa mashua
Takriban watu 4 wamefariki kufuatia ajali ya boti, iliyokuwa imewabeba kwenda kutafuta hifadhi nchini Australia kutoka Indonesia
Ajali hii imetokea huku mjadala mkali ukiendelea kuhusu sera mpya ya uhamiaji nchini Australia.
Boti yao ilizama katika ufuo wa kisiwa cha Java nchini Indonesia , ambacho ni kivukio cha watu wanaofanya biashara haramu ya binadamu.
Takriban watu 157 wameokolewa. Hata hivyo haijulikani ni wangapi wangali kupatikana.
Wakati huohuo, waziri wa uhamiaji wa Australia amesema kuwa atachunguza madai ya watu kudhulumiwa katika kituo chake cha usajili kisiwani Papua New Guinea.
Waziri mkuu Kevin Rudd alitangaza sera hiyo mpya ya kuzuia wahamiaji kuingia nchini humo huku uchaguzi mkuu ukikaribia.
Chini ya sera hiyo, wahamiaji wanaotafuta hifadhi nchini huo na ambao wanawasili kwa mashua , watarejeshwa katika kituo cha Papua New Guinea kwa uchunguzi zaidi kuhusu hali yao ya ukimbizi na ikiwa watapatikana kuwa wakimbizi basi watapewa hifadhi katika kisiwa hicho wala sio nchini Australia.
Australia imeshuhudia ongezeko la idadi ya watu wanaotafuta hifadhi na ambao wanawasili kwa boti katika miezi ya hivi karibuni.
Lakini wakosoaji wanasema kuwa Australia inakataa majukumu yake huku iyaachia nchi ambayo inastawi.
Bwana Rudd alisema kuwa kuzama kwa mashua inaonyesha umuhimu wa kubadili sera akisema kuwa serikali ililazimika kutuma ujumbe kwa watu wanaofanya biashara ya ulanguzi wa binadamu ili wakome kuingiza watu nchini humo kwa boti au mashua.

No comments:

Post a Comment