Msemaji wa Mamlaka ya
Chakula na Dawa, Gaudensia Simwanza (katikati)
akieleza jambo kwa waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari-Maelezo, kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari-Maelezo Zamaradi
Kawawa kushoto ni Salum Kindoli Mtaalam wa Maabara.
Picha zote na Hassan Silayo-MAELEZO)
MAELEZO
KUHUSU MAFANIKIO YA MAABARA YA CHAKULA
NA MIKROBIOLOJIA BAADA YA KUPATA ITHIBATI KWA KIWANGO CHA KIMATAIFA CHA ISO/IEC
17025:2005
Wakurugenzi
wa Idara ya Habari Maelezo,
Waandishi
wa Habari,
Mabibi
na Mabwana.
Ndugu wanahabari,
Napenda
kwa heshima na taadhima kutumia fursa hii kwa niaba ya Menejimenti ya TFDA na
wafanyakazi wote kwa ujumla kuwakaribisha katika mkutano huu. TFDA ni taasisi ya Serikali iliyopo chini ya
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyoundwa chini ya sheria namba 1 ya
Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 kwa
lengo la kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa,
vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya za wananchi.
Ndugu wanahabari,
TFDA
ilianza kazi rasmi tarehe 1 Julai, 2003 na kama taasisi nyingine ina dhima,
dira na falsafa zake kama ifuatavyo:-
Ni ukweli usiopingika kwamba vyakula, dawa,
vipodozi na vifaa tiba ni bidhaa nyeti na kila mmoja wetu ikiwa ni pamoja na
familia zetu tunazitumia kila siku. Hata hivyo, kama hazikudhibitiwa ipasavyo
matumizi ya bidhaa hizi yanaweza kuleta madhara makubwa ikiwa ni pamoja na
kusababisha ulemavu, kupoteza maisha na hata kudhoofisha uchumi wa nchi.
TFDA kama taasisi iliyopewa dhamana ya usimamizi wa
bidhaa hizo inahakikisha kwamba vyakula, dawa (ikiwa ni pamoja na dawa za
mitishamba), vipodozi na vifaa tiba vinavyouzwa katika soko la Tanzania
vinakidhi viwango vya usalama, ubora na ufanisi.
Hivi sasa TFDA inatambuliwa kwa kufanya kazi kulingana na viwango vya
kimataifa vya ISO 9001: 2008.
Ndugu wanahabari,
Moja kati
ya kazi muhimu za TFDA ni kufanya uchunguzi wa kimaabara wa sampuli za bidhaa
zinazodhibitiwa ili kurahisisha/kuwezesha kufanya maamuzi mbalimbali. Kupitia
uchunguzi wa kimaabara, TFDA hutegemea matokeo ya ukweli wa kisayansi (Scientific based evidence) katika kuamua
kusajili bidhaa, kuingiza au kutoa bidhaa nje ya nchi na pia katika kuamua
kuendelea kushikilia/kudumisha usajili wa bidhaa husika na kuziruhusu kuendelea
kuwepo katika soko.
Aidha,
kupitia uchunguzi wa kimaabara, TFDA huweza kubaini uwepo wa bidhaa bandia na
duni na hivyo kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa umma.
Kwa minajili hii Maabara ya TFDA ni chombo muhimu katika kuisaidia Menejimenti
kufanya maamuzi na hivyo kutimiza wajibu wa kusimamia usalama, ubora na ufanisi
wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na Vifaa tiba nchini.
Ndugu wanahabari,
Leo tumekutana hapa kwa lengo la kupeana taarifa
kuhusu mafanikio ya Maabara ya TFDA
katika kulinda afya ya wananchi. Mafanikio hayo ni kama ifuatavyo;
i.
Kutambuliwa
na Shirika la Afya Duniani (WHO)
Maabara
ya dawa ya TFDA ilifanyiwa ukaguzi na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwezi Mei
2005 na baadaye Septemba 2010 na kufanikiwa kukidhi vigezo, hivyo kutambuliwa
rasmi na WHO tarehe 18 Januari 2011.
Maana
yake ni kuwa Matokeo ya uchunguzi kupitia maabara hii yanatambuliwa kimataifa.
ii.
Kupata
ITHIBATI kwa kiwango cha ISO/IEC 17025:2005
Maabara
ya Chakula na Mikrobiologia ilifanikiwa kupata ITHIBATI kwa kiwango cha ISO/IEC 17025:2005 kutoka taasisi ya Southern African Development Community
Accreditation Services (SADCAS),
iliyotolewa tarehe 21 Septemba 2012.
Hii pia ina maana kwamba, matokeo ya uchunguzi
katika maabara hii yanatambuliwa na kukubalika kimataifa.
Cheti tulichopewa ni cha miaka mitano mpaka mwaka
2017, lakini kila mwaka wakaguzi toka SADCAS watakuwa wakikagua ili
kujiridhisha kwamba TFDA bado inakidhi kiwango cha ISO/IEC 17025:2005.
Ndugu
wanahabari,
Ni vema kufahamu kuwa Maabara hii ya TFDA ni miongoni mwa maabara nne (4) za Afrika ambazo zimepata ithibati kutoka SADCAS katika uchunguzi wa kimaabara kati ya 12, ambapo
nane (8) zikiwa ni Maabara zisizo za
udhibiti.
Vilevile ieleweke kwamba zipo Maabara chache
nyingine hapa nchini zinazofuata mfumo
huu ingawa si maabara za udhibiti.
Baada ya kufikiwa kwa mafanikio haya, Maabara hii
ya TFDA ilizinduliwa rasmi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, mnamo tarehe 18 Machi 2013.
Ndugu
wanahabari,
Faida zitokanazo na
maabara ya TFDA kutambuliwa kimataifa ni pamoja na;
(i)
Wananchi kupata uhakika wa bidhaa za chakula, dawa vipodozi na Vifaa tiba
zilizo kwenye soko
(ii)
Wazalishaji kupata maabara ya kuchunguza
bidhaa zao katika maabara inayotambulika
‘’competent labs’’ ili kupunguza hasara
ya kuzalisha bidhaa mbovu na kisha kuiharibu
(iii)
Kutokurudia matokeo ya uchunguzi kama maabara iliyo chunguza imepata Ithibati hii hupunguza gharama kubwa na muda wa
uchunguzi ‘’avoid expensive re-testing’’
(iv)
Kwa wazalishaji na wasambazaji kupata nafasi ya kuchunguza bidhaa zao katika
maabara zinazotambulika ‘’competent labs’’ na hivyo kutopoteza hadhi kwa bidhaa
wanazo zalisha/ kusambaza
Kutokana na
kutaambuliwa na shirika la Afya Duniani kwa maabara ya dawa na kupata ithibati
kwa maabara za chakula na mikrobiolojia, Mamlaka imeanza kupata wateja kutoka
nchi za nje na mashirika ya kimataifa. Nchi hizo ni pamoja na Kenya, Zambia, Rwanda,
Uganda, Ethiopia, Nigeria, Cameroon, Ghana na Botswana. Kwa kulitambua hili, TFDA iko katika hatua za mwisho
za kuandaa mpango maalumu wa kuboresha huduma za maabara (business plan) ili
kukidhi mahitaji ya wateja wa ndani na nje.
Mpango huu umepitia upya muundo wa maabara, taratibu za utoaji huduma,
mahitaji ya vifaa na wataalamu. Lengo
kuu ni kuongeza tija bila kuathiri dhima ya TFDA ya kulinda afya ya jamii.
Ndugu
wanahabari,
Tangu kuanzishwa kwa maabara ya TFDA mwaka 2003
hadi Machi 2013, Sampuli mbalimbali zimeweza kuchunguzwa katika maabara ya TFDA
kama ifuatavyo; chakula (5,173), dawa (6,163), vipodozi (307) na Vifaa tiba
(36).
Kupitia
mfumo wa Ufuatiliaji wa dawa (PMS) kwa lengo la kujiridhisha na usalama, ubora
na ufanisi wa dawa, katika kipindi cha Julai 2008 - Desemba 2012, jumla ya
sampuli 1,827 zilichukuliwa katika soko na kuchunguzwa katika maabara ya TFDA
ambapo sampuli 1,670 (97%) zilikidhi vigezo.
Aidha, kupitia Matokeo ya uchunguzi wa
kimaabara katika kipindi cha takriban miaka 10 sasa (2003 – 2013) bidhaa
mbalimbali duni na bandia ziliweza kubainika na kutolewa katika soko kama
ifuatavyo; bidhaa za chakula (84), bidhaa za dawa (71), bidhaa za vipodozi
2,764 na bidhaa za vifaa tiba (1).
Naamini uzoefu wa miaka takribani 10 tulio nao
katika uchunguzi wa kimaabara na upatikanaji wa ITHIBATI kutaendelea
kuifanya TFDA kufanya kazi kwa ufanisi zaidi katika kutekeleza mfumo huo wa utendaji kazi wa kimaabara ili
bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba zitakazouzwa kwenye soko la
Tanzania ziwe na viwango vinavyokubalika vya usalama, ubora na ufanisi.
Ndugu
wanahabari,
TFDA inatoa shukurani kwa ushirikiano ambao mmekuwa
mkiuonesha katika kutoa taarifa za kiudhibiti pale inapotokea pamoja na
kuelimisha jamii.
Rai yangu kwenu ni kuendelea kutumia kalamu zenu
katika kuwaondolea hofu wananchi kuhusu usalama na ubora wa bidhaa za chakula,
dawa, vipodozi na Vifaa tiba vilivyopo katika soko kutokana na mifumo thabiti
iliyowekwa na TFDA.
Aidha, wito kwa wananchi ni kwamba ikiwa mtu atabaini
au kuwa na shaka juu ya bidhaa hizo basi asisite kuwasiliana nasi kupitia ofisi
zetu za Makao Makuu na za Kanda zilizipo Extenal Mabibo, Mwanza, Arusha, Mbeya,
Dodoma na Ofisi za Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya au kutoa taarifa katika
kituo chochote cha polisi kilicho jirani naye.
No comments:
Post a Comment