Msanii Aunt Ezekiel |
Na Benedict Liwenga, Maelezo
WASANII nchini wameshauri kuwa na imani na Bodi ya Filamu na kuondokana na dhana potofu iliyojengeka juu ya Bodi hiyo kuwa haipo rafiki na wasanii.
Hayo yamesemwa leo, jijini Dar es Salaam na Msanii wa Filamu za Kiswahili Aunty Ezekiel katika kikao na Bodi ya Filamu wakati wa kupitia maeneo yalyohitaji marekebisho kwa filamu yake mpya ya “Scola”.
Aunt Ezekiel ameeleza kuwa amefurahishwa na Bodi ya Filamu Tanzania kwa kufanya majadiliano mazuri juu ya filamu yake kwa kubaini mapungufu baadhi yaliyopo na kumuelekeza cha kufanya.
“Nashukuru bodi wamekuwa waelewa ,wamenielekeza kurekebisha baadhi ya vipengele ili kuboresha filamu yangu naahidi kuirekebisha kwani vinarekebishika.”alisema Aunt Ezekiel.
Aidha Aunt Ezekiel ameomba radhi kwa kutoleta script yake ya filamu hiyo mpya ya SCOLA Bodi ya Filamu na amesema atakuwa akiwasilisha miswada yake kabla ya kutengeneza filamu zake. Aidha amewahakikishia watanzania kuwa atakuwa mfano bora katika kutengeza filamu bora na zenye maadili.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi hiyo Bi.Joyce Fissoo ameeleza kuwa kuna umuhimu wa wasanii kufata sheria na taratibu za filamu kabla ya kuanza kutengeneza na kuzitoa filamu zao ambapo sheria inawataka kuwasilisha mswada (script) Bodi ili na kupewa idhini yakuendelea na kazi hiyo.
“Wasanii mnatakiwa kuzingatia sheria na kuwasilisha script ili zikaguliwe na kupata ruhusa kwa mujibu na taratibu za sheria kabla ya kuanza kutengeneza filamu kwa sababu sheria Na 4 ya mwaka 1976 ya Filamu na Michezo ya kuigiza pamoja na kanuni zake zinaelekeza wasanii kutotoa au kutengeneza filamu kabla ya kupeleka mswada (script ) Bodi ya Filamu ili ipitiwe.
Aidha Katibu huyo amefafanua kuwa wasanii wanapotengeneza filamu kupitia script ambazo hazijakaguliwa kuna uwezekano mkubwa wakuwepo sehemu ambazo zinakiuka maadili ya mtanzania,ikiwepo uvaaji wa mavazi mafupi yaliyopitiliza kwa waigizaji wanawake,lugha mbaya na baadhi ya vitendo vingine visivyofaa kuoneshwa kwa umma.
Amewataka wasanii nchini kutengeneza filamu zinazozingatia maadili ya Kitanzania ikiwemo kutocheza picha zenye mavazi yanayoopitiliza kwa ufupi,kubana au zinazoonesha maumbile ya muigizaji mara kwa mara.
Kikao hiki pia kiliwashauri Bodi ya Filamu kukutana na wasnii wa kike ili kujadili masuala ya mavazi yasiyo nastaha, Bodi imeridhia ombi hilo.
No comments:
Post a Comment