TANGAZO


Tuesday, June 11, 2013

Maandamano zaidi dhidi ya wabunge Kenya


Hasira za waandamanaji zadhihirika kufuatia juhudi za wabunge kujiongeza mishahara
Mashirika yasiyo ya kiserikali yamefanya maandamano mengine mjini Nairobi Kenya kupinga jaribio la wabunge kujiongeza mishahara hata baada ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kusema kuwa hakuna pesa za kutosha kuwaongeza misahara wabunge hao.
Mashirika hayo yanataka wabunge kukubali mishahara waliyowekewa na tume ya kudhibiti mishahara ya wafanyakazi wa serikali. Kulingana na tume hiyo wabunge wanapaswa kupokea dola elfu sita kila mwezi lakini wanataka pesa hizo kuongezwa hadi dola elfu kumi au shilingi laki nane za Kenya.
Maandamano ya leo yanakuja siku kadhaa baada ya baadhi ya wabunge kusema kuwa tayari wamepokea mishahara ya shilingi lake nane na kupelekea tume hiyo kusema kuwa yeyote atakayepokea zaidi ya laki tano atalazimishwa kulipa pesa hizo.
Pia yanakuja siku tatu baada ya bunge kufutilia mbali sherehe zake za jubilee ambapo ilitarajiwa kuruhusu wananchi kujionea bunge.
Mmoja wa wandaaji wa maandamano hayo Bwana Boniface Mwangi, alisema kuwa waandamanaji walikuwa wanashinikizwa sana kuwa wasiandamane.
Mwangi aliandaa maandamano ya kwanza tarehe 14 mwezi Mei ambapo alileta Nguruwe nje ya majengo ya bunge na kuwafananisha na wabunge hao kama Nguruwe ambao ni walafi.
Wakati huohuo, majaji watatu wameteuliwa kusikiliza kesi zinapopinga hatua ya wabunge kutaka kujiongeza mishahara
Majaji hao Isaac Lenaola, Mumbi Ngugi na Weldon Korir, watasikiliza kesi hizo zilizowasilishwa na chama cha mawakili nchini Kenya na mwanaharakati Okiya Omtatah.
Jaji Lenaola alisema kuwa tume inayoshughulikia maslahi ya wabunge isidhubutu kuwalipa wabunge mishahara ya juu kuliko iliyokubaliwa na tume ya mishahara hadi kesi hizo zitakapokamilika.

No comments:

Post a Comment