SERIKALI imeandaa warsha
ya wazi ya siku mbili kwa wananchi ili kujadili na kutoa maoni kuhusu mpango
mpya wa ufatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ujulikanao kama 'Big Results Now'.
Hayo, yamesemwa na Kaimu
Katibu Mkuu Kiongozi Peniel Lyimo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo, ofisini kwake jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akielezea kuhusu maandalizi ya warsha hiyo.
Katibu Mkuu Lyimo, amesema kuwa warsha hiyo, itawapa nafasi wananchi kukutana na wataalamu
waliofanya kazi hiyo ana kwa ana pamoja na kuuliza maswali na kupata uelewa juu
ya miradi ambayo utekelezaji wake utaongeza kasi ya kukua kwa uchumi na
kuiwezesha nchi kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
“Serikali imeandaa
warsha ya wazi, ambapo matokeo ya uchambuzi wa kitaalamu yatawasilishwa ili
kutoa fursa kwa wananchi kuchangia na kutoa maoni juu ya miradi na program hizo
za maendeleo,” alisema Kaimu Katibu Mkuu.
Aidha, Katibu Mkuu huyo
ameeleza kuwa warsha hiyo itafanyika kwa siku mbili kuanzia Mei 24 hadi 25, 2013 katika Viwanja vya
Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam ambayo yatafunguliwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Ameeleza kuwa Serikali
imefanya uamuzi wa kuanzisha mfumo mpya wa ufuatiliaji na tathmini ua
utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele ya Mpango wa maendeleo wa miaka mitano
ambao unaanzia 2011 hadi 2016 ili kuboresha na kuharakisha utekelezaji wa Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Aliongeza kuwa mfumo huo
wa ufuatiliaji ni utaratibu ambao umeleta mafanikio makubwa katika nchi ya
Malaysia na unajulikana kwa jina la “Big Fast Result” (BFR),kwa Tanzania
utaitwa Big Result Now (BRN) ambapo utaratibiwa na kitengo maalum
kitakachoundwa chini ya ofisi ya
Waziri Mkuu.
Kwa upande wake Katibu
Mtendaji wa Tume ya Mipango Dk.Philip Mpango amesema kuwa mfumo huu utajikita
katika kuchambua kwa kina miradi iliyobainishwa katika mpango wa maendeleo wa
miaka mitano, kuainisha maeneo machache yatakayoleta matokeo makubwa haraka,kuandaa ratiba ya utekelezaji wa kila
mradi na kuzaidia katika utatuzi wa changamoto mbalimbali wakati wa
utekelezaji,ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu huru wa kupima utendaji kazi wa
viongozi wenye dhamana ya kutekeleza miradi na program za maendeleo.
Wananchi wametakiwa
kujitokeza kwenda kutoa maoni yao na kuangalia baadhi ya miradi ambayo ipo chini
ya mpango huo, ili kuweze kujifunza na kuongeza uelewaa juu ya utaratibu huo mpya ulioridhiwa na Baraza la Mawaziri kakita warsha iliyofanyika mjini Dodoma Oktoba 22-24, 2012.
No comments:
Post a Comment