TANGAZO


Wednesday, May 8, 2013

Waasi wa PKK waanza kuondoka Uturuki

Waasi wa PKK wa Uturuki

Wapiganaji waasi wa Kikurdi wameanza kuondoka kusini mashariki mwa Uturuki kwenda kwenye ngome zao nchini Iraq chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano, kimeeleza chanzo cha habari cha Wakurdi.
"Tunafahamu kwamba, wameanza kuondoka," Selahattin Demirtas, mwanasiasa wa Kikurdi aliyeshiriki katika mchakato wa amani ameliambia shirika la habari la AFP.
Chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi (PKK) kilitangaza mwezi uliopita kwamba, wapiganaji hao wataondoka kwa awamu kuanza mapema Mei .
Zaidi ya watu 40,000 wameuawa katika mapigano ya miaka 30 ya kuipinga Uturuki.
Gultan Kisinak, ambaye ni naibu kiongozi wa Chama cha Amani na Demokrasia (BDP) pamoja na Bwana Demirtas waeliambai shirika la habari la Associated Press kwamba, kundi la kwanza la wapiganaji limeanza kuelekea upande wa kaskazini mpakani na Iraq.
Inaaminika kwamba, chama cha PKK kinawapiganaji wanaofikia 2,000 ndani ya Uturuki na itawachukua muda wa miezi minne kwa wote kuondoka kabisa nchini humo.
Wanatarajiwa kuvuka mpaka kwa miguu na kuelekea kwenye ngome zao katika milima ya Qandil nchini Iraq.
Abdullah Ocalan kiongozi mkongwe wa PKK aliyeko gerezani nchini Uturuki, aliamuru kuondoka kwa wapiganaji wake mwezi Machi kama sehemu ya majadiliano ya amani na serikali ya Ankara.
Msemaji wa PKK, Bakhtiyar Dogan, ameliambia gazeti la Uturuki la Hawlati kwamba, kati ya wapiganaji 200 hadi 500 wataondoka siku ya Jumatano.
Amesema wapiganaji hao wataondoka kutoka maeneo ya Semdinli na Sirnak ya Uturuki wakiwa katika makundi matatu.
Kwa mujibu wa AFP, wapiganaji wa PKK walilalamika kuwa katika kilele cha siku ya kuondoka kwao, Uturuki iliongeza idadi ya wanajeshi wake eneo la mpakani na ilikua ikirusha ndege za doria.
Wamedai kuwa vitendo kama hivyo vinachelewesha mchakato wa amani na kuchochea uchokozi na mapigano.

Hata hivyo jeshi la Uturuki halijathibitisha iwapo hatua za ziada zimechukuliwa lakini limesema mapambano yake dhidi ya ugaidi yanaendelea.
Kaimu kiongozi wa PKK, Murat Karayilan, Aprili mwaka huu alionya kuwa wapiganaji wake watajibu na shughuli ya kuondoka ingesitishwa endapo wangeshabuliwa.
Wakati wa kuondoka mwaka 1999, jeshi la Uturuki liliwashambulia waasi hao na kuwaua wapiganaji wake 500.
Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, mara kadhaa ameahidi kuwa, jeshi halitamshambulia mpiganaji yeyote wa PKK atakayekuwa anaondoka.
Siku ya Jumanne, Bw. Erdogan alisema kuwa, kuweka silahachini ndio kiwe kipaumbele cha kwanza ili mchakato wa amani uweze kufanikiwa.

No comments:

Post a Comment