TANGAZO


Thursday, May 16, 2013

Maafisa wa usalama wa Misri watekwa nyara Sinai



Eneo la Sinai
Maafisa saba wa usalama wa Misri, wametekwa nyara na watu wasiojulikana katika Rasi ya Sinai , kwa mujibu wa maafisa wa Misri.
Maafisa hao , Polisi watatu na wanajeshi wanne walitekwa wakati wakisafiri katika basi dogo Kaskazini mwa Sinai mashariki mwa mji wa El Arish.
Watekaji nyara wanasemekana kudai kuachiliwa kwa jamaa zao wanaozuiliwa katika gereza la Misri
Ripoti zinaarifu kuwa viongozi wa kikabila wa Bedouin, wametakiwa kuingilia kati.
Rais Mohammed Morsi amewaita waziri wake wa ulinzi na waziri wa mambo ya ndani kwa mkutano wa dharura baada ya kutekwa nyara kwa maafisa hao.
Maafisa wanasema watu waliokuwa wamefunika nyuso zao waliteka teksi mbili nje ya mji wa el-Arish, na kuwakamata polisi na askari kisha wakarejea mjini Cairo.
Matukio mengi ya uhalifu yamekuwa yakiongezeka katika Kanda hiyo tangu alipong'olewa mamlakani rais Hosni Mubarak mwaka 2011.
Wanamgambo wa kiislam wamekuwa wakitumia eneo hilo kama ngome ya mashambulio dhidi ya vikosi vya usalama vya Misri na Israeli
Rasi ya Sinai imekuwa eneo lenye visa vingi vya uhalifu tangu rais Hosni Mubarak kung'olewa mamlakani mwaka 2011.
Kumekuwa na matukio kadhaa ambapo watalii kutoka nchi za kigeni wametekwa nyara katika eneo hilo.
Duru zinasema kuwa kawaida wao huachiliwa haraka lakini wahamiaji wengine kutoka nchi maskini wanaokwenda huko kutafuta maisha mazuri, wamewahi kutekwa nyara na kuteswa vibaya na watu wanaofanya biashara haramu ya binadamu eneo la Sinai

No comments:

Post a Comment