TANGAZO


Thursday, May 30, 2013

Daily Monitor hatimaye lafunguliwa


Gazeti la Daily Monitor nchini Uganda, limefungua ofisi zake leo baada ya kufungwa na maafisa wa polisi kwa zaidi ya wiki moja.
Gazeti hilo la binafsi, lilifungwa baada ya kuchapisha barua inayodai kuwa rais Yoweri Museveni anamuandaa mwanawe kumrithi kama rais .
Barua hiyo inayosemekana kutoka kwa generali wa jeshi, ilisema kuwa wale waliokuwa wanapinga mpango wa Museveni , huenda wakauliwa.
Taarifa ya serikali ilisema kuwa wamiliki wa gazeti hilo, wameelezea kusikitishwa kwa kuchapishwa kwa taarifa hiyo.
Setesheni mbili za redio zilizo chini ya kampuni ya Daily Monitor pia zilifungwa .
Wafanyakazi wa gazeti hilo walisema kuwa polisi waliokuwa wamezingira ofisi za kampuni hiyo kwa siku kumi na moja zilizopita, wameanza kuondoka katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti hilo kwenye mtandao wafanyakazi wa gazeti hilo, wameweza kurejea kazini huku polisi wakionekana kuzifungua ofisi hizo.
Gazeti la Red Pepper pia lilifungwa kwa kuripoti madai hayo.
Museveni amekuwa mamlakani tangu mwaka 1986 na uchaguzi unatarajiwa kufanyika mwaka 2016.
Kumekuwa na tetesi kuwa mwanawe Museveni, Bregedia Muhoozi Kainerugaba, anaandaliwa kuweza kumrithi Museveni atakapoondoka mamlakani .
Hata hvyo serikali imekanusha madai hayo na kusema kuwa haina mpango wowote kama huo.

Msako kuendelea

Mapema wiki hii, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi pamoja na virungu wakati wakiandamana nje ya ofisiu za gazeti hilo.
Maafisa wa utawala wanasema kuwa walitaka ushahidi kuhusu namna gazeti la Daily Monitor lilivyopata barua hiyo ya siri , inayodaiwa kuandikwa na Generali David Sejusa, ambaye yuko nje ya nchi.
Kwenye taarifa ya serikali, msako uliofanywa tarehe 20 mwezi Mei mwaka 2013 uliamrishwa kwa sababu ilisemekana kuwa katibu mkuu wa usalama wa ndani, ambaye barua hiyo ilikuwa inatumwa kwake pamoja na maafisa wengine walionuiwa kupokea barua hiyo ambayo hata hiuvyo hawakuweza kuipokea. Baadaye ilijulikana kuwa ni kampuni ya Daily Monitor pekee iliyokuwa na barua hiyo
Rais Museveni na wakuu wa kampuni ya vyombo vya habari ya Nation , inayomiliki Monitor, walikutana siku ya Jumapili kujadili hali ya gazeti la Daily Monitor.
Walikubaliana kuwa wachapishe taarifa walizo na uhakika nazo na ambazo vyanzo vyake vinaweza kuaminika.
Pia walikubaliana kuwa maakini na taarifa ambazo zinaweza kusababisha hali ya taharuki , chuki za kikabila na kusababisha utovu wa usalama.

No comments:

Post a Comment