TANGAZO


Monday, March 18, 2013

Marekani: "kweli tunaye Ntaganda "

 

Ntaganda ajisalimisha
Hatimae Marekani imethibitisha kuwa Muasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jenerali Bosco Ntaganda, amejisalimisha katika ubalozi wake mjini Kigali, Rwanda.
Taarifa hiyo ya Marekani inasema kuwa Ntaganda ameomba ahamishwe hadi katika Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa ICC huko the Hague.
Ntaganda aliyeanzisha maasi nchini Congo ameshitakiwa katika mahakama hiyo ya ICC na anakabiliwa na mashitaka ya kuwajumuisha watoto katika jeshi, mauaji na ubakaji.
Jenerali Ntaganda mwenyewe anakanusha madai hayo yote.
Marekani imesema kwa wakati huu inashauriana na serikali kadhaa ili kufanikisha ombo hilo la Jenerali Ntaganda ahamishwe hadi mahakama ya ICC.
Awali Serikali ya Rwanda ilikuwa imetangaza kuwa Jenerali huyo muasi anayetuhumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amejisalimisha katika ubalozi wa Marekani mjini Kigali, Rwanda.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo amesema taarifa walizonazo ni kuwa Kiongozi huyo muasi yuko chini ya ulinzi wa Marekani katika ubalozi wake.
"Tumefahamishwa hii leo (Jumatatu) kuwa Bosco Ntaganda ameingia Rwanda na kujisalimisha katika Ubalozi wa marekani hapa Kigali", amesema Louise Mushikiwabo
Jenerali Ntaganda amekanusha mashitaka yanayomkabili katika mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai ICC kwamba anahusika na uhalifu wa kivita na ule dhidi ya binadamu.

No comments:

Post a Comment