Waziri wa Ushirikiano wa EAC Samwel Sitta |
Na Joyce Kasiki, Dodoma
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samweli Sitta amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kutumia nafasi zao kukabiliana na vurugu zinazotokea katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza mara baada ya kufungua mkutano wa mwaka wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Sitta alisema kuwa viongozi hao, wanatakiwa kutokuwa waoga, waweze kukabiliana na hali hiyo, ambayo imekuwa ikitokea kwa sababu mbalimbali zikiwemo za udini.
"Hawa wapo kwa ajili ya kumwakilisha Rais, hivyo wana kila sababu ya kutumia madaraka waliyopewa katika kukabiliana na vurugu hizo, hakuna sababu ya wao kuwa waoga katika jambo hili," alisema Sitta.
Sitta alisema kuwa, kadri nchi inavyokuwa watu wanataka kutumia vibaya fursa za uhuru, hali ambayo imesababisha kuleta wasiwasi huku wengine wakitumia vurugu chini ya imani zao za dini.
Alisema kuwa wapo baadhi ya Wakuu wengine wa Mikoa ni waoga, jambo ambalo linafanya washindwe kuchukua maamuzi mapema na wanachotakiwa ni kuondoa woga huo kwa kushughulikia jambo, likiwa bado bichi na si kusubiri vurugu zitokee na kuleta maafa.
Alisema kuwa kama viongozi hao, watafanya hivyo, vitendo vya mauaji ya kidini vinavyo hatarisha amani nchini, vitapungua na kuwatoa hofu wananchi.
Kwa upande wake, Rais wa TLS, Francis Stolla, alisema kuwa huduma za kisheria hapa nchini bado ni ghali, hali inayosababisha baadhi ya wananchi kushindwa kupata huduma za kisheria pindi wanapozihitaji.
Alisema kuwa kunatakiwa kujenga mazingira ya kuwezesha watu wasio na uwezo ili kupata huduma hizo kwa gharama nafuu.
No comments:
Post a Comment