Na Baltazar Mashaka, Mwanza
Februari 7, 2013
MELI ya abiria ya Mv. Victoria, mali ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), jana imenusurika kuteketea kwa moto ikiwa katika Gati la bandari ya Mwanza Kaskazini, baada ya cheche za moto kulipuka kutoka katika chumba cha mizigo.
Meli hiyo, ambayo hufanya safari zake kati ya Mwanza na mjini Bukoba, mkoani Kagera ilikuwa ikipakia mizigo katika gati la bandari ya Kaskazini tayari kwa safari ya kuelekea mkoani huko usiku wa kuamkia leo.
Kwa mujibu wa kuli mmoja bandarini hapo (jina linahifadhiwa), aliyeshuhudia tukio hilo, alieleza kuwa moto huo ulizuka katika chumba cha shehena ya magodoro na mito (Quation) zikisafirishwa kwenda Bukoba .
Alisema moto huo, ulizuka majira ya saa 9:10 alasiri ambapo chanzo kinaelezwa kuwa kilitokana na fundi mmoja aliyekuwa akichomelea ndani ya chumba cha mizigo na cheche za moto kushika shehena ya magodoro na mito iliyokuwa ndani ya chumba hicho.
Hata hivyo kikosi cha Zimamoto kiliwasili mapema na kufanikiwa kuzima moto huo ambao tayari ulishatekeza sehemu ya shehena hiyo,mali ya Zulfikar na mwenzake aliyetajwa pia kwa jina moja la Ogunya, ambapo gazeti hili lilishuhudia shehena baadhi ya mito na magodoro hayo iliyoungua ikipakuliwa kutoka ndani ya meli .
Aidha Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Vyombo vya Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) Kanda ya Ziwa, Japhet Loisimaye,alisema utawala ulipaswa kufahamu kuwapo kwa matengenezo ili kuepusha ajali kama hiyo.
Alisema kutokan a na kazi hiyo uongozi ulipaswa kuwa na mtu wa pili ambaye angekuwa na mtungi wa maji ya kuzima moto pale kama ilivyotokea na kudai kwa vile hilo halikufanyika uongozi umefanya uzembe na kusababisha hasara kwa wasafirishaji wa mizigo iliyoungua moto.
“Fundi alikuwa akichomelea kwenye gamla ya mizgo upande wa pili kwenye ukuta wa meli.Cheche ndiyo chanzo cha moto huo kulipuka baada ya kushika kwenye shehena ya Magodoro,kwenye chumba ambacho ni mbali na sehemu wanayokaa abiria ndani ya meli,”alisema Loisimaye na kuongeza;
“Kwa upande wa usalama wa meli haina tatizo, ni kule ilikokuwa ikichomelewa lakini haiwezi kusitisha safari zake kutokana na kuwa imekukaguliwa na kupewa cheti cha ubora.Isipokuwa wakati wanachomelea alipaswa kuwapo mtu wa pili wa kupambana na moto (Fireman ) ambaye alipaswa kuwa na mtungi wa maji ya kuzima moto,lakini hakuwepo na huo ni uzembe wa utawala.”
Alisema kampuni ilipaswa kufahamu kinachondelea , endapo taarifa ya ukaguzi wa moto ikifikishwa kwao na ikabainika walifanya uzembe, suala hilo litafikishwa kwenye vyombo husika kwa hatua zaidi.
Aidha Kaimu Meneja wa wa MSCL aliyetajwa jina moja la Kapinga, hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo badala yake akadai wenye jukumu hilo ni Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto ambaye ndiye msemaji wa masula ya moto na si wamiliki wa meli.
“Hapa utapata double standard ,taarifa inatoka Zimamoto hata kama wewe ni mmiliki .No news to follow na kama meli ilikuwa na matizo nahodha ndiye anapaswa kuzungumzia meli yake.Hata hivyo vuta subira,kama ni suala la muda hata mimi nimecha kazi ya Mahakamani kesho na jaji hataweza kunisikiliza kwa sababu ya dharura hii,”alisema Kapinga
Habari zaidi kutoka chanzo cha kuaminika zinasema kuwa meli hiyo kwa muda wa miaka miwili sasa haijafanyiwa matengenezo na ilipaswa ipelekwe kwenye chelezo ili kufanyiwa matengenezo makubwa.
Kwamba meli hiyo imechakaa vibaya na imekuwa ikiwekea viraka kwa kuzibwa kwa kutumia mbao ,ambapo Jumanne juzi whinch ilikatika wakati ikipakia mizigo na kukandamiza shehena ya mizigo ya viungo vya pilipili (Chill source) mali mfanyabishara aliyetajwa kwa jina moja la Zulfikar au Zully.
“SUMATRA wasijikoshe na hili, meli ni mbovu na wao walikuwa wametoa maelekezo ipelekwe kwenye dock (chelezo) sababu kwa miaka miwili sasa haijafanyiwa matengenezo.Sisi tumeshauri sana lakini uongozi hausikii , Jumanne pia nusura moto uwake kwani wanakochomelea kuna mabomba ya kupitisha mafuta na kulikuwa na shehena ya rangi ya mafuta ,”alisema mtoa habari huyo.
Alisema kuwa uchomeleaji wa gamla za meli hiyo unafanywa bila kuwepo kwa mtu mwenye mtungi wa maji ya kuzimia moto endapo itajitokeza hitilafu wakati wa kuchomelea na endpo hatua hazitachukuliwa wakati wa kuchomelea, iko hatari ya meli hiyo kuungua moto.
No comments:
Post a Comment