Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akionnyesha Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, baada ya kuizindua rasmi huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja leo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizindua Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Na-Maelezo
Zanzibar
14/11/2012
Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa jamii inahitaji kuelimishwa zaidi juu ya
umuhimu wa uzazi wa mpango kwa maendeleo ya nchi sambamba na kutunza afya ya
jamii hasa kwa akina mama na watoto.
Kauli hiyo
imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
katika hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani ya mwaka 2012
iliyofanyika katika viwanja vya skuli ya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja,
ambako alimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.
Ali Mohd Shein.
Amesema jamii
bado haijatoa umuhimu unaostahiki katika matumizi ya njia za uzazi wa mpango,
hali inayopelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la watu ambalo huathiri harakati za
maendeleo na afya ya jamii.
“Taarifa
zinaonesha kwamba Zanzibar hivi sasa inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 1.3
milioni, wanaoongezeka kwa kasi ya asilimia 3.1 kwa mwaka ambapo idadi ya watu
katika kila kilomita moja ya mraba imefikia watu 496 mwaka 2011”, ilieleza
sehemu ya hotuba hiyo ya Dkt. Shein iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa
Rais.
Amefahamisha
kuwa bado vifo vya mama wajawazito viko juu duniani lakini vimepungua kwa upande
wa Tanzania na Zanzibar hasa kwa kina mama wenye umri mdogo na wanaokabiliwa na
tatizo la umaskini.
“Kwa Tanzania
katika mwaka 2004/05 idadi ya vifo ilikuwa 578 kwa kila akina mama waja wazito
100,000 na kupungua kidogo hadi kufikia vifo 454 mwaka 2010. Hata hivyo kwa
Zanzibar vifo vya akina mama vimepungua kutoka vifo 473 mwaka 2006 hadi vifo 281
mwaka 2011, kwa kila kina mama 100,000 kwa takwimu za hospitali”,
alifafanua.
Amesema
mafanikio hayo yametokana na juhudi za serikali katika kuimarisha huduma za afya
kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo za pepopunda na shurua, sambamba na
kuimarisha huduma za afya ya uzazi katika hospitali mbali mbali.
Ametoa wito
maalum kwa Wazazi kuwaozesha watoto zao kuanzia umri wa miaka 20 na kuendelea
ili wamalize masomo yao kwani elimu ni ufunguo wa Maisha.
Kwa upande wao
wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kwa kuona umuhimu wa huduma ya uzazi na kuamua kutoa huduma hiyo bila ya
malipo.
Mwakilishi
Mkaazi wa Shirika la Idadi ya watu (UNFPA) Tanzania bibi Mariam Khan
amesema bado suala la uzazi wa mpango linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni
pamoja na wanajamii kuona ugumu juu ya matumizi ya njia za uzazi wa
mpango.
Amesisitiza kuwa
Mashirika ya Kimataifa ya UN na UNFPA yataendelea kuziunga mkono jitihada
zinazofanywa na Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar ili
kuhakikisha jamii inapata uelewa na kudumisha uzazi wa mpango.
Amefahamisha
kuwa uzazi wa mpango ni muhimu katika kusaidia kukuza kipato cha wanafamilia,
sambamba na kuwaendeleza watoto katika makuzi bora, na wito kwa jamii kutoa
fursa zinazostahiki kwa akina mama na watoto ili kusaidia harakati za maendeleo
kwa jamii.
Kwa upande wake
Waziri wa Afya Mhe. Juma Duni Haji amesema wameamua kufanya uzinduzi huo katika
Mkoa wa Kaskazini Unguja, ili kutoa uelewa zaidi kwa wakaazi wa Mkoa huo ambao
ni miongoni mwa mikoa inayofanya vibaya katika suala la uzazi wa
mpango.
Amesema
akinamama na watoto wanahitaji kulindwa kiafya, na kuwataka wazazi hasa wa kiume
kushirikiana kikamilifu katika suala la malezi na makuzi ya watoto
wao.
Mapema akitoa
muhtasari wa ripoti hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya
Maendeleo Khamis Mussa amesema kimsingi ripoti hiyo imeelezea juu ya changamoto,
faida na haki za binadamu katika uzazi wa mpango.
Amesema uzazi wa
mpango ni miongoni kwa haki za binadamu lakini imeelekezwa zaidi kwenye haki za
kifamilia, ili wanafamilia waweze kupanga juu ya idadi na umri wa kupishana kwa
watoto, ili kuepuka mimba zisizotarajiwa.
“Inakisiwa kuwa
kiasi cha mimba milioni 80 zinapatikana bila ya kutarajiwa duniani, huku nusu ya
mimba hizo zikitolewa, jambo ambalo ni hatari katika uzazi”. Alidokeza Katibu
Mkuu huyo.
Kauli mbiu ya
mwaka huu ni “Uzazi wa Mpangilio katika ukuzaji Uchumi.”
No comments:
Post a Comment