Wanachama wa Shirikisho la Wanafunzi wa Chama Cha Mapinduzi, Vyuo Vikuu, Dar es Salaam, wakionesha bango linalowatataka Watanzania kuendelea kuwaondoa watendaji wabovu kwenye Chama hicho na Serikali, wakati wa mkutano wao jijini juzi. (Picha na Kassim Mbarouk)
SHIRIKISHO la Wana-CCM, Vyuo Vikuu, Dar es Salaam, wamesema kuwa hawatosita kuwatoa viongozi waliopo madarakani kwenye Chama Cha Mapinduzi na pia Serikali, iwapo watabaini watendaji hao ni mzigo kwa Serikali na chama kwa ujumla.
Aidha, Shirikisho hilo, limeelezea kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete kutokana na usikivu wake na kuwateu mawaziri wapy, waliowataka kuchapa kazi na kuwaondoa mara moja watendaji wabovu, waliowapachika majina ya magamba, bila kuwaonea haya.
Shirikisho hilo la Wana - CCM Vyuo, Dar es Salaam, limesema kwamba kama Mawaziri hao watashinda kuwawajibisha watendaji wao wabovu, basi wao hawatasita kamwe kuwafuata na kuwatoa maofisini mara moja.
"Tunamshukuru Rais wetu Kikwete kwa uteuzi wake wa Wakuu wa Wilaya, tunawaomba vijana muende mkachape kazi, msituangushe vijana wenzenu, hatutasita kuwatoa ofisini mkichemka, nendeni mkayavue magamba yakajifiche kwenye magwanda," ilisema sehemu ya taarifa ya Shirikisho hilo, iliyotiwa saini na Mwenyekiti wake Asenga Abubakar na kusambazwa kwa waandishi wa habari.
Aidha, taarifa ya Shirikisho hilo, iliyotolewa juzi wakati wa mkuatno wake uliofanyika Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, imelaani na kupinga vikali kile walichokiita ajenda ya siri ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ya kutaka kuwagawa Watanzania kwa Uzanzibar na Utanganyika na Ukanda wa Kaskazini na kuitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua hatua kali dhidi ya waliowaita waropokaji vinginevyo taarifa imesema kwamba ikifika Jumamosi ijayo, bila kuchukuliwa hatua stahili kwa watu hao, Shirikisho hilo, halitosita kuwaomba Watanzania wote wapenzi wa amani, kuandamana mpaka msajili huyo wa Vyama vya Siasa kuitisha kwa ajili ya kulinda umoja wao.
Taarifa hiyo pia ilimtaka Mbunge wa Jimbo la Ubungo, kupitia Chadema, John Mnyika kutekeleza ahadi alizowaahidi wananchi wa Ubungo, ilizozitaja kuwa ni ubovu wa barabara na ukosefu wa maji safi kwa matumizi mbalimbali.
Pia taarifa ya Shirikisho hilo, iliwataka viongozi wa Chadema kuwataja Wabunge 70 pamoja na Mawaziri waliotajwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kuwa wameomba kujiunga na chama hicho na kumaliza kwa kuwaeleza viongozi hao kwamba wanaendea na mazungumzo na mmoja wa Mjumbe wao wa Kamati Kuu kwa ajili ya kujiunga na CCM hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment