Malalamiko makali yamezidi kutolewa kuhusu mauaji ya zaidi ya watu 90 katika mji wa Houla, Syria.
Kati ya watu hao walikuwamo watoto wadogo.
Na kumetolewa wito kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likutane.
Na mjini Damascus, serikali kwa mara nyengine tena imekanusha kuwa ilihusika.
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Damascus, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Nchi za Nje, Jihad Makdissi, alikanusha kabisa kuwa wanajeshi wa serikali walihusika na mauaji ya Houla siku ya Ijumaa.
Alieleza kwamba kulitokea mapambano Ijumaa jioni baina ya wanajeshi na "magaidi" waliokuwa na silaha, ambapo wanajeshi watatu waliuwawa.
Alisema kuwa mamia ya watu waliokuwa na silaha nzito, pamoja na mizinga, walikwenda Houla kushambulia na kuchoma nyumba, na kupiga risasi vichwani watoto, wanawake na wanaume.
Alisema jeshi la serikali halina mtindo huo, limekula kiapo kuwalinda raia.
Alisema jeshi la serikali katika eneo hilo halikuwa na mizinga.
Piya alisema kuwa mashambulio hayo yamefanywa wakati huo, kusadifiana na mkutano wa Baraza la Usalama na ziara inayotarajiwa, ya Kofi Annan, kwa sababu waliofanya hivo wanataka kuchafua utaratibu wa kurejesha amani.
Alisema Baraza la Usalama linafaa kuuliza nani anayapatia silaha na kugharamia yale aliyoyaita "makundi ya magaidi".
No comments:
Post a Comment