TANGAZO


Tuesday, May 29, 2012

Rais wa Somalia ashambuliwa

Rais wa Somalia
Rais wa serikali ya mpito ya Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed ameponea shambulio lililofanywa na wapiganaji wa kiisilamu katika ziara yake kwenye eneo lililotwaaliwa na majeshi ya Muungano wa Afrika karibuni.
Msafara wa Rais Sheikh Sharif ulishambuliwa kwenye barabara ya kutoka eneo la Afgoye kuelekea mji mkuu Mogadishu. Mji Afgoye ulidhibitiwa na majeshi ya Muungano wa Afrika wiki jana.
Maafisa wa Somalia wamesema Rais huyo wa mpito ameweza kurejea Mogadishu akiwa salama.Wapiganaji wa Al Shabaab na ambao walijjiunga na mtandao wa Al-Qaeda mwaka huu wamekiri kuhusika na shambulio hilo.
Mji wa Afgoye umekuwa ngome kuu ya kundi la Al-Shabaab baada ya kundi lenyewe kuondoka Mogadishu, na wametumia eneo hilo kushambulia mji mkuu.
Mwanajeshi mmoja wa serikali ya Somalia aliuawa na wengine wanne wakajeruhiwa wakati Al Shabaab walipoufiatulia risasi msafara wa Rais kwenye barabara kati ya Afgoye na Mogadishu.
Msemaji wa wanajeshi wa AMISOM Paddy Ankunda amesema wanajeshi wa Muungano wa Afrika waliwazidi nguvu washambuliaji hao.

No comments:

Post a Comment