Nahodha wa Bolton Kevin Davies amesema kuzungumzia kuhusu klabu yao kujitoa katika mashindano ya Kombe la FA "hayana maana" wakati huu kila mtu akiwa anatafakari afya ya Fabrice Muamba.
Muamba, mwenye umri wa miaka 23, bado yu- mahututi baada ya kuanguka na kuzirai uwanjani wakati wa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham.
Kumekuwa na ushauri Bolton ijitoe katika mashindano hayo kwa vile wachezaji wa Bolton hawajisikii vizuri kurejea tena kucheza katika uwanja wa White Hart Lane.
Lakini Davies ameiambia BBC:"Tumeulizwa swali kama hilo na nadhani bado yote naona hayana maana."
Ameongeza: "Hadi tutakapopata taarifa zaidi kuhusu hali ya Fabrice, sidhani kama kuna jambo jingine tunalofikiria.
Mechi hiyo ya mzunguko wa sita kuwania Kombe la FA ilifutwa baada ya kuchezwa kwa dakika 41 siku ya Jumamosi, wakati Muamba alipoanguka na kuzimia uwanjani akiwa peke yake.
Davies amesema amekuwa akizungumza na meneja wake Owen Coyle pamoja na mwenyekiti Phil Gartside - na klabu itaamua iwapo waendelee kucheza katika Kombe la FA au la "katika siku chache zijazo".
Mshambuliaji huyo ameongeza kusema: "Sote tunampenda Fabrice. Namheshimu sana kutoka alipotoka hadi alipofikia hivi sasa."
Davies amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na daktari anayemtibu Fabrice na yeye pamoja na Coyle wamekuwa wakitoa taarifa za maendeleo ya hali ya Muamba kwa wachezaji wenzake.
Coyle amesema: "Wamefurahishwa na kutiwa moyo sana na namna walivyoungwa mkono. Tumeona picha kutoka kila kona ya dunia.
Unapowaona wachezaji wa timu ya Real Madrid na Gary Cahill, wakiwa wamevalia fulana, huku David Beckham akituma ujumbe, hiyo yote inaonesha wamemthamini Fabrice kama binadamu.
No comments:
Post a Comment