Didier Drogba umaliziaji wake maridadi umeihakikishia ushindi ingawa mwembamba Chelsea dhidi ya Stoke City iliyokuwa ikicheza pungufu ya mchezaji mmoja katika pambano la kwanza la Roberto di Matteo kusimamia akiwa meneja wa muda Chelsea katika Ligi Kuu ya England.
Chelsea mipira yao iligonga mwamba mara mbili lakini iliwabidi wawe waangalifu kuikabili Stoke City iliyokuwa ikijihami vizuri.
Lakini Drogba hatimaye akamaliza kazi baada ya kumzunguka mlinda mlango Asmir Begovic baada ya kupokea pasi ya Juan Mata na kupachika bao lake la 100 tangu aanze kucheza Ligi Kuu ya England.
Hali ya kusua-sua kwa Liverpool kwenye ligi imeendelea tena baada ya kuchapwa na timu iliyoonesha ari ya kusaka ushindi ya Sunderland.
Baada ya kosakosa za kipindi cha kwanza, Sunderland walifanikiwa kuongoza kwa kupachika bao baada ya mkwaju wa Fraizer Campbell kuzuiwa na mlinda mlango Pepe Reina kabla ya Nicklas Bendtner kuuwahi na kuutumbukiza wavuni.
Liverpool waliwaingiza Steven Gerrard na Andy Carroll lakini mabadiliko hayo hayakuzaa matunda kwa upande wa wao.
Sunderland walijihami vyema kulinda bao lao moja dhidi ya Liverpool ambao nusura wangesawazisha.
Junior Hoilett akifunga mabao mawili ameisaidia timu yake ya Blackburn kupanda juu kutoka eneo la hatari la kuteremka daraja na kuicha Wolves wakicheza uwanja wa nyumbani wakiendelea kusuasua eneo la kuteremka daraja wakiwa nafasi moja tu kutoka mkiani.
Mashabiki wa Wolves walifanya maandamano kabla ya mchezo dhidi ya Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu yao ya Wolves Jez Moxey kwa kumteua Terry Connor kushikilia nafasi ya umeneja na hatimaye wakashuhudia timi yao ikiporomoka kwa kuonesha kiwango cha chini.
Hoilett alifunga bao lake la kwanza baada ya kumiliki mpira wa kimo cha mbuni na kuachia mkwaju kutoka upande wa kona na kuingia moja kwa moja wavuni.
Na baadae mshambuliaji huyo akafanikiwa kufunga bao lake la pili kwa mkwaju wa yadi 25 mara tu baada ya kuanza kipindi cha pili.
Kufungwa huko kumeicha Wolves nafasi ya 19, nafasi moja tu kutoka mkiani wakiwa wamepata ushindi wa mchezo mmoja tu katika mechi 14 za Ligi zilizopita.
Bao la kwanza la Andreas Weimann la Ligi Kuu ya England liliipatia ushindi Aston Villa dhidi ya Fulham waliokuwa wakicheza kwa kiwango cha juu na hatimaye wakamaliza kwa huzuni katika uwanja wa Villa Park.
Villa walimiliki mchezo katika kipindi cha kwanza huku Gabriel Agbonlahor nusura angepachika bao.
Marc Albrighton alipiga mkwaju uliogonga mwamba katika dakika za mwanzo za kipindi cha pili na baadae Damien Duff wa Fulham mkwaju wake nao ukagongwa mwamba. Hadi mwisho Aston Villa 1 Fulham 0.
Meneja wa QPR Mark Hughes aliachwa asifahamu la kufanya baada ya kushuhudia timu yake ikinyimwa ushindi baada ya bao la dakika za mwisho la Ivan Klasnic kuipatia ushindi wa mabao 2-1 Bolton.
QPR ilitakiwa kuwa mbele kwa bao moja kipindi cha kwanza lakini mpira wa kichwa aliochonga Clint Hill haukuhesabiwa bao licha ya mpira kuonekana umevuka mstari.
Bolton iliongoza kwa bao la kwanza lililofungwa kwa kichwa na Darren Pratley kabla Djibril Cisse kusawazisha kwa mkwaju wa karibu, ingawa baadae picha za televisheni zilizokuwa zikirudiwa zilionesha alikuwa ameotea.
Lakini bao la dakika za mwisho la Klasnic aliyepokea pasi murua kutoka kwa Ryo Miyaichi na kufanikiwa kumpita mlinda mlango Paddy Kenny, liliitoa Bolton kutoka eneo hatari la kuteremka daraja.
No comments:
Post a Comment