Jaji mmoja nchini Marekani amesema kuwa kampuni kubwa ya mafuta, BP, imekubali kuwapa fidia, kabla ya kesi kufika mahakamani, watu wanaoishtaki kampuni hiyo kwa sababu ya mafuta yaliyomwagika kutoka kisima cha mafuta cha BP, katika Ghuba ya Mexico, miaka miwili iliyopita.
Kisima cha mafuta cha BP kikiwaka moto kwenye bahari ya Ghuba ya Mexico, Marekani
Watu 11 walikufa, huku mamilioni ya mapipa ya mafuta yalimwagika katika pwani hiyo ya Marekani, baada ya bomba moja la mafuta kulipuka.
Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza Jumatatu, lakini sasa imeahirishwa.
Wengi walioathirika ni wavuvi waliokosa riziki wakati wa mafuta yalipotapakaa baharini.
BP ilisema imetoa fidia, lakini haimaanishi kuwa imefanya kosa katika ajali hiyo.
Kampuni bado inakabili mashtaka kutoka serikali ya Marekani na wenye hisa kwenye kampuni hiyo.