Baraza la kijeshi linalotawala Misri limetuhumu makundi ya kigeni kwa kusaidia kifedha maandamano ya mitaani dhidi ya utawala.
Marekani imeonya kuwa itapitia upya misaada ya Marekani kwa Misri, ikiwa nchi hiyo haitaheshimu haki za mashirika yasiyo ya kiserikali.
Msemaji wa serikali ya Marekani Victoria Nudland amesema Marekani "imepatwa na wasiwasi sana na taarifa hizo" na ilikuwa ikitafuta "ufafanuzi" kutoka kwa serikali ya Misri.
Kundi la wanaharakati wa haki za binaadam la Human Rights Watch limetoa wito kwa Misri kufuta mashtaka dhidi ya wafanyakazi hao wa mashirika yasiyo ya kiserikali.
"Msaada kutoka nje ndio tegemeo lao. Serikali ya kijesi ya Misri sasa inatumia mbinu zilizotumika na Zimbabwe na Ethiopia kunyamazisha sauti huru," limesema kundi hilo.
Tangazo hilo limekuja katika siku ya nne ya ghasia mitaani nchini Misri huku kukiwa na hasira ya jinsi mamlaka zilivyoshindwa kukabiliana na matukio kwenye viwanja vya mpira wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu 74.
Majeshi ya usalama yalirusha mabomu ya kutoa machozi kwa maelfu ya waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe huku wakielekea katika jengo la wizara ya mambo ya ndani mjini Cairo.
Wamarekani 19 ni miongoni mwa wanaoshtakiwa.
Wanatuhumiwa kwa "kuunda matawi ya mashirika ya kimataifa nchini Misri bila ya leseni kutoka serikalini" na pia kwa "kupokea fedha kutoka nchi za nje kinyume cha sheria," limeripoti shirika la habari la AFP.
Mtoto wa waziri wa usafiri wa Marekani Ray LaHood anaaminiwa ni miongini mwa wanaokabiliwa na mashtaka hayo ya uhalifu.
Sam LaHood anaongoza ofisi ya shirika la IRI iliyopo Misri na ni miongoni mwa wafanyakazi kadhaa wa kigeni kunyimwa ruhusa ya kuondoka Misri, wiki moja iliyopita.
IRI na NDI, mashirika yanayohusishwa na vyama vya kisiasa vya Republican na Democrat vya Marekani, ni miongoni mwa mashirika 17 yanayopokea fedha kutoka nje na ambayo ofisi zao zilivamiwa na waendesha mashtaka mwezi Disemba.
No comments:
Post a Comment