Carlos Tevez akata rufaa kupinga kukatwa mshahara wa wiki sita
Tevez alitozwa faini ya paundi milioni 1.2 baada ya kupatikana na hatia ya utovu wa nidhamu na rufaa yake baadae kutupwa na bodi ya klabu.
Mzozo huo unaoendelea umemgharimu Tevez hasara ya paundi milioni 9.3 ikiwa ni kukosa mshahara, faini na marupurupu mengine.
Imefahamika hata hivyo mchezaji huyo hatarajii kuondoka Manchester City kabla ya dirisha la usajili mdogo kufungwa siku ya Jumanne usiku na uamuzi wake wa kukata rufaa utazidi kuvuruga uwezekano wake kurejea katika klabu hiyo.
Mzozo huo ulianza wakati Tevez alipotozwa faini ya kukatwa mshahara wa wiki mbili baada ya meneja wake Roberto Mancini kumtuhumu mshambuliaji huyo alikataa kuingia akiwa mchezaji wa akiba wakati Manchester City walipopambana na Bayern Munich katika mpambano wa Ubingwa wa Ulaya, ingawa Tevez alidai hakukuwa na maelewano.
Aliondoka kuelekea Amerika Kusini na akatozwa faini ya mshahara wa wiki sita kufuatia mashtaka ya utovu wa nidhamu, wakati ilifahamika alikuwa hajalipwa mshahara wake unaokadiriwa kufikia paundi 200,000 kwa wiki, tangu mwezi wa Novemba.
Tevez hajaichezea Manchester City tangu tarehe 21 mwezi wa Septemba walipoifunga Birmingham.

No comments:
Post a Comment