Medani ya Tahir
Maelfu waadhimisha mwaka mmoja wa mapinduzi ya kiraia Misri.

Maelfu ya wananchi wa Misri wamekusanyika katika Medani ya Tahrir mjini Cairo kuadhimisha mwaka mmoja wa mapinduzi yaliyomng'oa madarakani Rais Hosni Mubarak.
Baadhi yao wanasheherekea mafanikio ya vyama vya kiislamu katika uchaguzi wa kwanza baada ya kuondoka kwa Mubaraka huku wengine wakihimiza mageuzi zaidi ya kisiasa.
Sheria za hali ya hatari ambazo zimetumika kwa muongo mzima zimeondolewa ili kuadhimisha siku hiyo.
Bw Mubarak anakabiliwa na mashtaka ya kuamuru waandamanaji wauawe madai ambayo anayakanusha.
Mamia ya watu waliohukumiwa adhabu ya vifungo jela na mahakama za kijeshi walitazamiwa kuachiliwa siku ya jumatano katika hatua inayodhaniwa kuwa itawaridhisha waandamanaji. .
Usiku wa Jumanne maelfu ya watu walipiga kambi katika medani Tahrir, nembo ya maandamano ya mwaka jana wakiungwa mkono baadaye na maelfu wengine wakiwakilisha mirengo mipya ya siasa za kiislamu na za wastani.
Mwaandishi wa BBC Jon Leyne, akiwa mjini Cairo, anasema hali imekuwa ya utulivu hadi sasa ikionekena kama ni karamu kubwa mitaani badala ya maandamano ya kisiasa.