William Ruto akiwa na Joshua Sang, mstari wa mbele

Wagombea wawili wa urais nchini Kenya wana kesi ya kujibu juu ya uhalifu dhidi ya binadamu kufuatia vurugu za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imeamua.
Naibu Waziri mkuu Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri William Ruto wote wanakabiliwa na mashtaka.
Ni miongoni mwa wakenya wanne mashuhuri - wote ambao wamekanusha madai hayo - wanaokabiliwa na mashtaka.
Rais wa Kenya amewaomba raia wawe watulivu baada ya uamuzi huo.
" Nchi hii yetu tukufu imekuwa na changamoto kubwa," Mwai Kibaki alisema katika taarifa yake.
Bw Kenyatta - mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya na mtu ambaye ameorodheshwa kama mmoja ya watu matajiri - anakabiliwa na mashtaka yeye pamoja na mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura.
Wawili hao, wote washirika wa rais, wanashutumiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwemo mauaji na mateso.
Waziri wa zamani wa Elimu William Ruto na mwandishi wa habari Joshua arap Sang wanakabiliwa na mashtaka katika kesi tofauti, kwa kuwa walikuwa wapinzani wa Bw Kibaki wakati wa uchaguzi wa mwaka 2007. Mahakama ya mjini the Hague iliamua hakuna ushahidi wa kutosha wa kuanzisha kesi dhidi ya maafisa wengine wawili.
Zaidi ya watu 1,200 waliuawa katika wiki kadhaa za vurugu na watu takriban 600,000 wakalazimishwa kukimbia makazi yao. Wengi bado wanakaa katika makambi ya muda.