Ofisa Maendeleo ya
Vijana Wilaya ya Chamwino Bw. Denis Vagela (kushoto) akizungumza na Vijana wa
kikundi cha Wajasiriamali wa Wilaya ya Chamwino wanaojishughulisha na
utengenezaji wa Sabuni za maji, Batiki na ufundi walipotembelewa kwa ajili ya
kuangalia mradi wao leo Mkoani Dodoma. Katikati ni Mwezeshaji kutoka Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa, na aliyekaa ni Afisa
Vijana Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga.
Kijana Samwel Nagija kutoka kikundi cha vijana cha Chachu ya Maendeleo Dodoma kinachojishughulisha na utengenezaji wa mashine za kusaga na kukoboa, mashine za kutengeneza matofali, mashine za kukamua alizeti, na ujenzi wa vitanda na madawati ya chuma akiendelea na ujenzi wa mashine ya kusaga leo Mkoani Dodoma.
Mwenyekiti wa kikundi
cha vijana cha Iringa Promise Keepers Bw. Rashid Magule (kushoto) kinachojishughulisha
na ufundi Selemala akielezea namna kikundi chake kilivyofaidika na mkopo
unaotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Wanaomsikiliza
kutoka kulia ni Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Bibi Ester Riwa, anayefuata ni Afisa Maendeleo ya Vijana Bi. Amina Sanga
na wapili kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw.Laurean Masele. (Picha na: Genofeva Matemu – Maelezo,
Dodoma)
Na Genofeva Matemu
Tarehe 15/01/2015
VIJANA kutoka kikundi
cha Iringa Promise Keepers chenye wanachama 6 wanaojishughulisha na ufundi
Selemala wameishukuru Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
unaosimamiwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuwapatia mkopo
wa shilingi laki tatu mwaka 2007 ambao umeinua na kusababisha mradi wa kikundi kupanuka na kuwa mkubwa.
Kauli hiyo imetolewa na
Mwenyekiti wa kikundi hicho Bw. Rashid Magule walipotembelewa na wawezeshaji
kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na maafisa kutoka ofisi
ya Mkoa wa Dodoma kukagua miradi ya vijana leo Mkoani Dodoma.
“Kikundi cha Iringa
Promise Keepers kinaishukuru Serikali kwa kutufaidisha na mkopo wa shilingi
laki tatu kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana tuliopatiwa mwaka 2007 ambao
ulikua kama mtaji katika kikundi chetu hivyo kupanuka na kuwa na mtaji wa
shilingi milioni nne unaotuwezesha wanakikundi kupata kipato cha kuweza
kuendesha maisha yetu” alisema Bw. Magule.
Hata hivyo Bw. Magule
ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
kuendelea kukipatia mkopo kikundi chake kwani bado wanakikundi wanahitaji
kujiendeleza zaidi na kuwaendelezo vijana wenzao wanaohitaji utaalamu kutoka
kwao hivyo kuomba kupatiwa mkopo wa shilingi milioni mbili kwa ajili ya
maendeleo ya kikundi hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa
Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya kilichopo chini ya Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Bw. Laurean Masele amewapongeza wanakikundi kwa jitihada
kubwa walizozifanya na kuweza kutumia mpoko mdogo waliopata kusimamia na
kuendeleza mradi wao kwa kushirikiana.
Bw. Masele amewashauri
wanakikundi kufanya kazi kwa ushirikiano huo huo huku wakisimamia malengo
waliyokusudia kwa kutumia ujuzi walionao kwani vijana wakiwezeshwa wanaweza.
Naye Afisa Maendeleo ya
Vijana Mkoa wa Dodoma Bw. Tumsifu Mwasamale amewapongeza wanakikundi wa Iringa
Promise Keepers kwa maendeleo waliyonayo na kuwataka kutafuta eneo lao binafsi
kwa ajili ya shughuli zao kwani mradi wao unahitaji nafasi kubwa na ya wazi
itakayosaidia kuonyesha bidhaa wanazozalisha katika jamii.
No comments:
Post a Comment