Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile (katikati), akikagua michoro ya jengo la Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii wakati alipotembelea ujenzi wa maabara hiyo unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kulia), akikagua jengo la Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii wakati aliootembelea kukagua ujenzi huo leo jijini Dar es Salaam. kushoto ni Mkurugenzi wa Ugavi na Manunuzi Wizara ya Afya Bw. Castro Simba.
Muonekano wa jengo la Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii liliopo jijini Dar es Salaam likiwa bado linaendelea na ujenzi.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (katikati), akipata maelezo kutoka kwa Mchunguzi wa Dawa na vipodozi Gerald Sambu (kulia), wakati alipitembelea TFDA leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi TFDA Bi. Agness Kijo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katikati akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA wakati alipotembelea mamlaka hiyo leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Bi. Agness Kijo.
Na WAMJW- Dar es Salaam
UJENZI wa Maabara ya Afya ya Jamii ya Taifa inayohusiana na magonjwa ya mlipuko unatarajia kukamilika ifikapo Julai mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa ziara yake ya kuangalia hali ya ujenzi wa maabara hiyo jijini Dar es salaam.
"Mpaka hivi sasa asilimia 60 ya ujenzi imekamilika hivyo namsisitiza Mkandarasi kwamba Serikali haitaongeza muda wa ziada mpaka kufikia Julali 9 mwaka huu tuwe tumeshakabidhiwa jengo hili" alisema Dkt. Ndugulile
Aidha, Dkt. Ndugulile alisema kuwa Maabara hiyo ya Afya ya Jamii ya Taifa ni kwa ajili ya kupima sampuli ya magonjwa ya mlipuko na itakuwa ni maabara kubwa Afrika yenye kiwango cha ubora wa BS3 ambayo imegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 7. 6.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya ukandarasi ya WCEC Injinia Edwins Shittindi amesema kuwa ujenzi huo ulitakiwa uwe umekamilika Oktoba mwaka jana badala ya Julai 2018.
"Tulitakiwa kukabidhi hiki jengo Oktoba 2017 lakini kutokana na vifaa ya kazi tulivyoviagiza kuchelewa kuwasili tutajitahidi mpaka kufikia Julai 9 mwaka huu tuwe tumekabidhi jengo" alisema Eng. Shittindi.
Sambamba na hilo Dkt. Ndugulile ametembelea Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA na kuwataka waangalie sana watu wanaotangaza vipodozi vyao kwenye mitandao ya jamii na kuandaa utaratibu husika kuhusu bidhaa hizo.
"Kila kukicha kuna matangazo mengi sana kwenye mitandao ya jamii yanayohusiana na vipodozi hivyo mnatakiwa kuchukua tahadhari na kufuatilia kwa ukaribu kuhusu ubora wa bidhaa zao" alisema Dkt. Ndugulile.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa TFDA wanatakiwa kuhakikisha ubora wa dawa , chakula pamoja na vipodozi unastahili ili watanzania waweze kutumia bidhaa zenye usalama zaidi.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile leo ametembelea maeneo mbalimbali ya TFDA ikiwemo sehemu ya usajili wa Dawa, maabara na kuweza kuongea na Uongozi wa Mamlaka hiyo.

No comments:
Post a Comment