TANGAZO


Thursday, March 22, 2018

MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI ZAMNYIMA MTOTO WA KIKE FURSA ZA KUPATA HAKI YAKE YA MSINGI YA KUENDELEZWA

Sehemu ya Wanafunzi kutoka shule sita za Jiji la Tanga wakifuatilia elimu ya kampeni ya kutokomeza mimba za utotoni Nchini.  
Kipeperushi.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu Bw. Mathias Haule kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo, Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Alicia elimu ya madhara ya ndoa na mimba za utotoni kwa wanafunzi wa shule za Msingi kutoka Jiji la Tanga. 
Wanafunzi Nasra Nyambukah na Moza Bandawe wa Shule ya Msingi Changa wakiwakilisha wenzao kutoka ujumbe kwa njia ya picha kuhusu kampeini ya kutokomeza mimba Za utotoni.

Na Anthony Ishengoma--Tanga 
HALI ya mimba za utotoni hapa Nchini imeendelea kuongezeka na kumnyima fursa mtoto kike kupata haki yake ya msingi kuendelezwa.


Akiongea na wanafunzi kutoka shule sita za jiji la Tanga katika washa ya siku moja kwa wanafunzi hao kuhusu kampeni ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto Bwana Mathias Haule amesema Elimu ndio njia sahihi kutimiza ndoto za mtoto wa kike. 

Bwana  Haule ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia zinaonesha kuwa jumla ya Wanafunzi 5,053 wameacha shule hapa Nchini kwa ajili ya mimba za utotoni.

Ametaja kuwa mimba 4,426 kwa mujibu wa takwimu hizo kuwa ni kutoka shule za Sekondari na 627 ni kutoka   shule za Msingi, takwimu hizi ni za mwaka 2016.

Aidha ameitaja Mikoa ya Mbeya(380) Mwanza(372), Kilimanjaro(348), Dodoma(308), na Ruvuma(300) kuwa na idadi kubwa za wasichana walioacha shule kwa sababu ya mimba.

Aidha Bw.Haule ameongeza kuwa serikari imebaini sababu za mimba mashuleni ni kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu malezi chanya,umuhimu wa mtoto kike kusoma, mila na desturi na umasikini wa familia.

Wakati huo huo Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Tanga Bi.Mwatumu Dossi amesema kwa mwaka 2017 jumla ya wanafunzi wa sekondari 20 walipata ujauzito. 


Ametoa wito kwa wazazi na walezi wa Jiji la Tanga kuwa karibu na watoto wao ili kuwapatia elimu ya Afya na jinsia ikiwemo kuacha kuwaoza wasichana katika umri mdogo.

Shule zilizo shiriki kampeni ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni ni shule za msingi za jiji la Tanga ambazo ni Shule ya Msingi Changa,Juhudi,Chumbageni,Kisosora na shule binafsi ya Changa English Medium. 

No comments:

Post a Comment