Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akiongea na wawakilishi wa wananchi, watumishi na Watendaji wa Halmashauri ya Mji Korogwe (hawapo pichani). Waziri Makamba amesisitiza umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na hifadhi ya mazingira kwa ujumla wake.
Baadhi ya wawakilishi wa wananchi, watumishi na
Watendaji wa Halmashauri ya Mji Korogwe wakimsikiliza Waziri Makamba alipofanya
ziara ya kikazi kutembelea Halmashauri hiyo, kusikiliza na kujionea changamoto
za kimazingira na kuainisha namna bora ya kukabiliana nazo.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Mhe. January Makamba ameendelea na ziara yake maalumu ya kukagua shughuli
mbalimbali za kimazingira nchini na hii leo amepokea taarifa ya hali ya mazingira katika
Halmashauri ya Mji Korogwe na Same.
Akimkaribisha Waziri Makamba,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya hiyo Bw. Hillary Ngonyani amesema kuwa katika
kutekeleza sheria ya mazingira zoezi la uzoaji na utupaji wa taka ngumu na taka
maji umewekewa mkakati maalumu na kutekelezwa kikamilifu pia usafi wa mazingira
umefanyika kwa kufanya ukaguzi wa nyumba hadi nyumba na kutoza faini kwa
wananchi wasio na vyoo.
Aidha Bw. Ngonyani amebainisha
kuwa wananchi wanaokiuka taratibu hizo hushtakiwa kwenye mabaraza ya kata na
kupewa muda maalumu wa kujenga vyoo, kusisitizwa kuvitumia pia kuamriwa
kusafisha mazingira yao chini ya uangalizi wa maafisa afya.
Bw. Ngonyani amesema kuwa wananchi
wamekumbusha pia kutofanya shughuli za maendeleo kando ya mito na vyanzo vya
maji ili kupunguza athari kwa mazingira, na kuunda kwa kamati za mazingira.
Katika hatua nyingine Bw.
Ngonyani ameinisha changamoto zinazojitokeza katika Halmashauri ya Korogwe mji
kuwa ni pamoja na Ukosefu wa wakaguzi wa Mazingira na athari za mabadiliko ya
tabianchi yanayosababisha vipindi vya mvua kubadilika na kuongezeka kwa joto.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. January Makamba amesema kuwa ni vema
rasilimali za nchi hii zitunzwe kwa faida ya sasa na vizazi
vijavyo."hatuwezi kufanikiwa kama tutaharibu mazingira" Makamba
alisisitiza.
Waziri Makamba amesema ofisi yake
ya imedhamiria kuchukua swala la mazingira kwa uzito wa kipee ikiwa ni pamoja
na kuweka hifadhi ya mazingira katika mipango ya maendeleo." Uwekezaji
wote lazima uende sambamba na hifadhi ya mazingira"
Aidha, uongozi wa Halmashauri ya
Mji Korogwe imetakiwa kuwachukua hatua kali wananchi wote wanaofanya shughuli
za kibinadamu katika vyanzo vya maji, kwa kutumia sheria ya Mazingira ya mwaka
2004 na ile ya maji ya mwaka 2009. Waziri Makamba amesema kuwa ofisi yake iko
katika hatua za mwisho za kuteua wakaguzi wa mazingira 200 ambao watapata
mafunzo na kusambazwa katika Halmashauri mbali mbali nchini.
Pia Waziri Makamba amesema kuwa
katika kikao kijacho cha Bunge Ofisi ya Makamu wa Rais itatoa waraka juu ya
usimamizi na uchimbaji wa mchanga nchini pamoja na umiliki wa
"Chain-saw" kwa lengo kuweka utaratibu utakaowezesha kutambua na
kutoa vibali maalumu kwa shughuli hizo ili kulinda mazingira.
Akiwa Wilayani Korogwe Waziri
Makamba amechangia mifuko 200 ya sementi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za
ujenzi katika Halmashauri ya Korogwe Mjini.

No comments:
Post a Comment