Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akimsikiliza
Meneja wa Mamlaka ya Bandari Kanda ya Ziwa, Bw. Abel Moyo, alipokagua gati ya
Bandari ya Bukoba, mkoani humo jana.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa mmoja wa Afisa Fedha kutoka Mamlaka ya Bandari (TPA), katika Bandari ya Bukoba alipokagua utendaji wa bandari hiyo na kubaini utaratibu mbovu wa ukusanyaji mapato.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiongea na mafundi wanaofanya ukarabati katika bandari ya Bukoba, alipokagua utendaji wa bandari hiyo Mkoani Kagera.
Baadhi ya
Watumishi wanaofanya kazi katika taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mkoani Kagera, wakimsikiliza Waziri wa Wizara hiyo,
Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani), alipooongea nao mkoani humo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mkoani Kagera, mara baada ya kuongea nao na kuwaeleza mikakati mbalimbali ya WIzara hiyo.
SERIKALI imewatoa wasiwasi wakazi na wafanyabishara wa Kanda ya Ziwa Victoria kuwa iko
katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za ujenzi wa meli mpya kubwa na
ya kisasa ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua mizigo tani 300, magari 25 na
madaraja matatu kwa ajili ya sehemu ya kukaa abiria.
Akizungumza na
waandishi wa habari mara baada ya kukagua bandari ya Bukoba, mkoani Kagera, Waziri
Profesa Mbarawa amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo umechelewa kutokana na
kukosa sifa kwa Makandarasi wawili waliojitokeza mwanzoni kwa ajili ya
kutekeleza mradi huo wa ujenzi.
“Nataka kujenga
meli ya kisasa ili kuweza kufupisha safari kutoka masaa 10 hadi matano kutoka
Bukoba hadi Mwanza na hivyo kufanya usafiri wa majini kuwa wa kuaminika na
salama”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Waziri
Mbarawa amefafanua kuwa kutokana na utendaji mbovu wa bandari hiyo anatarajia
kuleta wafanyakazi makini kwa ajili ya kupitia taaria za kifedha za utoaji na
usafirishwaji wa mizigo bandarini hapo.
Naye, Meneja wa
Mamlaka ya Bandari Kanda ya Ziwa, Bw. Abel Moyo ameiomba Serikali kufanya ukarabati
wa Meli nchini hasa zilizopo Kanda ya Ziwa ili kuweza kuondoa adha wanazozipata
wakazi wa mikoa hiyo.
Katika hatua
nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua Shirika la Posta mkoani humo na kuahidi
kupeleka wakaguzi wa ndani kwa ajili ya kukagua na kujiridhisha juu ya mapato
na matumizi ili kubaini ubadhilifu unaofanywa na watendaji wa Posta.
“Tunataka Posta
iwe safi na kupunguza changamoto zinazoikabili kwani ni Shirika kubwa na lenye
Rasilimali nyingi ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuinua mapato ya Shirika
hilo”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Akiwa katika
ofisi za Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoani humo, Waziri Prof. Mbarawa
ameuagiza Wakala huo kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa katika utengenezaji
wa magari yanayokuja kupata huduma katika karakana yao.
Kwa upande
wake, Meneja wa TEMESA, Eng, Zephrine Bahyona amemuomba Waziri kusaidia
kusisitiza Taasisi za Serikali kupeleka magari yao kwenye karakana zao na
kulipa madeni kwa wakati ili kupunguzia Wakala huo mzigo wa madeni kutoka
katika taasisi hizo.
Waziri
Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi wilayani Bukoba, mkoani Kagera ambapo
ametembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Taasisi zilizo chini
ya Wizara yake.
(Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano)

No comments:
Post a Comment