TANGAZO


Monday, February 20, 2017

PROF. OLE GABRIELI: TUNATAMANI IFIKE MAHALI WATANZANIA WAKIWEKE KISWAHILI KWENYE ROHO ZAO

Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel

Na Immaculate Makilika- Maeloezo
SERIKALI imesema inatamani kuona watanzania wanakiweka  kiswahili kwenye roho zao kwa kufikiri na kuzungumza lugha hiyo katika maeneo na shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa ili kukienzi pamoja na kuipa heshima inayostahili.

Akizungumza katika kipindi cha Je tutafika?  kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Channel ten, Katibu Mkuu,  Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel  alisema kuwa “Tunatamani ifike mahali kila mtanzania aone fahari kuongea lugha ya kiswahili,  hii itasaidia kuipa hadhi lugha hiyo kitaifa na kimataifa na hatimaye kuifanya lugha ya kiswahili kuwa bidhaa ili iweze kuuzwa”. Alisema Prof. Ole Gabrieli.

Ambapo  aliongeza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Habari imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuikuza lugha hiyo ikiwemo Baraza kiswahili Tanzania  kutoa kamusi mpya yenye maneno zaidi ya milioni moja na nusu, na zaidi ya istilahi 40.

Aidha, Profesa Ole Gabriel, alimpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuzungumza lugha ya kiswahili katika mikutano mbalimbali ya kimataifa, kwani hatua hiyo inasaidia kuikuza lugha hiyo na kuwavutia watu wengi zaidi kuizungumza kwa vile ni lugha inayounganisha watanzania pamoja na wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

” Lugha ni nyenzo muhimu ya kuhifadhi utamaduni, kwasababu utamaduni ndio namna tunayoishi na tunavyofikiri, hivyo watanzania tunatakiwa kufikiri na kuzungumza lugha ya pamoja ambayo kila mmoja ataelewa”.Alisema Prof. Ole Gabrieli.

Alitoa wito kwa watanzania kuwa na utamaduni wa kuongea lugha ya kiswahili ikiwa ni pamoja kuwafundisha watoto wao kuzungumza lugha hiyo kwa ufasaha.

Katika hatua nyingine Prof. Ole Gabrieli aliviomba vyombo vya habari nchini kuandaa vipindi  na vipindi mbalimbali vyenye lengo la kukuza lugha ya kiswahili kwa kuielekeza jamii juu ya matumizi  sahihi ya lugha hiyo.

No comments:

Post a Comment