TANGAZO


Monday, February 20, 2017

MAKALA:“HIFADHI YA TAIFA YA VISIWA VYA RUBONDO YANG’ARA ONGEZEKO LA WATALII”

Baadhi ya ndege mbalimbali wapatikanao katika Hifadhi ya Visiwa vya Rubondo

Na Judith Mhina- Habari Maelezo
IDADI ya watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Visiwa vya Rubondo imeongezeka kutoka watalii 452 kwa kipindi cha miaka 10 na kufikia 879 ndani ya mwaka mmoja, kutoka Julai 2015 mpaka Juni 2016.

Katika mahojiano maalum na Idara ya Habari MAELEZO, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi  hiyo Bw Ignace Gara  alieleza kuwa kati ya  watalii 879 waliotembelea hifadhi hiyo  525 ni kutoka nje ya nchi na 354 ni wa ndani. Aidha, kwa mwaka 2005 Julai mpaka Juni 2015 watalii 452 waliotembelea hifadhi hiyo wageni kutoka nje walikuwa ni 380 na wa ndani 72.

Bw Gara alifafanua kuwa  sababu kubwa ya ongezeko la watalii  ni pamoja na hatua ya uongozi kuitangaza hifadhi hiyo hasa  kupitia mitandao ya kijamii na uwepo wa migodi mingi katika kanda ya ziwa kama vile Migodi ya dhahabu ya Geita, Kahama na Buzwagi ambapo baadhi wa watumishi wa migodi hiyo wakiwemo wageni hutumia muda wa mapumziko kutembelea hifadhi hiyo.

Aidha, alitaja zoezi la  wataalamu wa wanyama pori kutoka Ulaya la kuwafundisha Sokwe mtu waliopo hifadhini kuzoea binadamu  kuwa ni miongoni mwa sababu za ongezeko hilo la watalii katika hifadhi hiyo.
Nzohe jike, mnyama ambaye anapatikana katika hifadhi ya visiwa vya Rubondo pekee nchini.

Bw. Gara amesema: “Rubondo ni nyumbani kwa aina pekee ya mnyama Nzohe hapa Tanzania wenye asili ya Afrika ya Kusini, ndege aina 400, samaki aina 13, Sokwe mtu  wa asili ya Afrika ya Magharibi na misitu minene mikubwa ya asili ya Kongo.

“Hifadhi ina utajiri mkubwa wa aina mbalimbali za ndege na samaki kama Sato, Sangara, Ngege, Mbiru, Furu, Ningu, Kuyu, Mbofu au Hongwe, Domodomo au Mbete, Soga,  Gogogo,  Kambale mumi, Kambale mamba au Kamongo, na Dagaa”. Baadhi ya aina samaki alieleza bw. Gara kuwa wanakuwa wakubwa hadi kufikia hadi kilo 100.

Hifadhi ya Rubindo inasifika kwa kuwa ni makaazi ya aina nyingi za ndege wakiwemo   Zumbuli, Chechelee na Taisamaki. Pia   ni makazi ya aina nyingi ya ndege wa majini na fukwe zilizojaa rasilimali za uoto wa asili wenye harufu nzuri ya kipekee.

Aidha uwepo wa mnyama pekee katika hifadhi za Tanzania Nzohe  na Pongo ambao huvinjari katika fukwe mwanana za visiwa vya Rubondo, ‘fish maji’  na  upande wa eneo la kulala watalii Tourist Bandaz, ni kati ya vivutio vikubwa vinavyofanya watalii wengi wa nje na ndani kutembelea hifadhi hii.

Aliongeza kwa kusema : “Kichocheo kikubwa kwa ustawi wa wanyama na ndege katika hifadhi hii ni upatikanaji wa malisho, maji, matunda asilia, vipepeo, wadudu na mbegu za nafaka asilia kwa mwaka mzima. Kwa hivyo ukiwa ndani ya kisiwa utaona mandhari nzuri ya ziwa Victoria”.
Nzohe dume, mnyama ambaye anapatikana katika hifadhi ya visiwa vya Rubondo pekee nchini. 

Akielezea historia ya Hifadhi ya Taifa ya visiwa vya Rubondo Bw Gara amesema “Historia ya hifadhi imetokana na umuhimu wa kuhifadhi wanyama katika kisiwa hicho ambacho wakaazi wake walijulikana kama Banyarubondo ambao walilazimika kuondolewa 1964 ili kupisha hifadhi kufuatia tangazo la waziri mwenye dhamana ya masuala ya maliasili”

Kwa mujibu wa Bw Gara kazi ya kuwaondoa wananchi hao ilikamilika mwaka 1965 baada ya wananchi hao kulipwa fidia na mwaka uliofuata (1966) Rubondo ilitangazwa kama pori la akiba na miaka 10 baadaye, yaani mwaka 1977 ikapandishwa daraja na kuwa hifadhi ya taifa. 

Ni vyema kueleza hapa pia kuwa uamuzi huu wa serikali wa kuanzisha hifadhi hiyo ulichangiwa pia na matokeo ya utafiti uliofanywa na Shirika la Frankfurt Zoological Society la Ujerumani uliobaini hatari ya baadhi ya wanyama kutoweka duniani wakiwemo wanaopatikana katika kisiwa hicho. 

Muikolojia wa hifadhi Bw Wickson Kibasa amesema miaka ya 1960, dunia ilianza kupata wasiwasi kuwa baadhi ya wanyama wangeweza kutoweka dunia. Hivyo, wataalam wa Ikolojia waliangalia uwezekano wa kuhamisha baadhi ya wanyama kama sokwe mtu, tembo na wengine kuwapeleka nchi za Ulaya ikiwamo Ujerumani, lakini baada ya kufananisha/kulinganisha uhalisia wa mazingira na uoto wa asili wa Afrika Mashariki wakapendekeza sehemu pekee duniani ya kuhifadhi wanyama hao na wanapoweza kuishi sawa na maeneo yao ya asili ni Rubondo. 

Bw Kibasa alifafanua kwa kusema, wakati katika maeneo mbalimbali ya hifadhi barani Afrika   ikiwemo Tanzania, baadhi ya wanyama kama tembo wanapotea kwa ujangili, hali ni tofauti katika Hifadhi ya Rubondo. Kila mwaka tembo waliopandikizwa wanaongezeka na wanyama kama, twiga, sokwe mtu, nzohe, ngedere weusi, weupe, mamba na viboko  na wanyama wengine walipandikizwa Rubondo wanaongezeka.

Mkuu wa Hifadhi Bw Gara, alihitimisha kwa kusema: “Ili kuondoa  changamoto za uvamizi, ujangili na uharibifu wa mazingira  Hifadhi imejikita katika kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa namnukuu:

“Kutoa elimu ya uhamasishaji wa jamiii kulinda na kuheshimu mipaka yote ya vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi nchini kwa lengo la kuondokana na migogoro mingi iliyokuwa ikijitokeza baina vijiji vya jirani na hifadhi”.

Waziri Mkuu alitoa maagizo haya, alipokuwa kwenye ziara yake Mkoani Manyara hivi karibuni na hifadhi yetu inatekeleza kikamilifu. Pia alisisitiza utakelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuongeza na kuboresha mazali ya samaki katika maeneo owevu au chepechepe ili kuwaletea wananchi uhakika wa chakula na  kipato.

Katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kitengo cha Ujirani mwema cha Rubondo “Kinatoa  elimu ya uhifadhi katika jamii zinazopakana na hifadhi, kupitia elimu hiyo wananchi wamekuwa wakielimishwa kuhusu madhara ya uvuvi haramu katika ziwa Victoria na mbinu za uvuvi endelevu ndani ya ziwa”. amesema Bw David Kadomo, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ujirani mwema.

Aidha, “Hifadhi kwa kushirikiana na maafisa uvuvi katika wilaya zinazopakana na hifadhi yetu, tumekuwa tukiwaelimisha wananchi na kuhimiza utunzaji wa ardhi oevu kwenye mialo za ziwa Victoria”.

Akifafanua mkakati huo Bw Kadomo amesema hifadhi: ‘Imeandaa mpango kwa kushirikiana na wananchi katika mialo ya Bulongero kata ya Izumacheli wilaya ya Geita, Kabiga kata ya Maisome wilaya ya Sengerema, Kasenyi kata ya Ikuza wilaya ya Muleba na Mwerani  kata ya Mganza wilaya ya Chato katika kuboresha na kuongeza vituo vya mazalia ya samaki katika mialo hiyo.

Matarajio ya Hifadhi ni kuboreshwa kwa mazalia ya samaki na kuanzisha vituo mbalimbali kando kando mwa ziwa ili, wananchi kuzalisha samaki kwa wingi kama azma ya serikali ilivyokusudia na kuondoa changamoto ya kutoweka kwa samaki wenye uzito mkubwa unaotakiwa viwandani,  hii itapunguza kama si kuondoa kabisa,  kasi ya watu kuja kufanya uvuvi kwenye maeneo ya Hifadhi.

Bw Kadomo alimalizia na kusema: “Kitengo cha Ujirani Mwema kinaandaa ziara za makundi mbalimbali ya jamii kuja kutembelea hifadhi na kuona vivutio mbalimbali ndani ya hifadhi. Makundi haya yamekuwa yakihusisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari zinazo jirani na hifadhi”.

Aliendelea kwa kusema:“Makundi mengine ni viongozi wa serikali za vijiji na kata zinazopakana na hifadhi”.

Hifadhi ya Rubondo,  kijografia ipo Mkoa wa Geita,   imezungukwa na visiwa 11 vidogo vidogo ambapo ni sehemu ya hifadhi,   kuna majabali makubwa 2; moja upande wa kaskazini  na  lingine upande wa kusini  ndani ya misitu minene ya asili ya Kongo.

Hifadhi ya Taifa ya visiwa vya Rubondo ipo jirani na visiwa kadhaa vya makazi ambayo ni Mizo, Nyamitundu, Chitende, Katera, Iroba, Chambuzi, Munyila, Makosi, pamoja na Izilambula. Rubondo ni hifadhi pekee nchini Tanzania na Barani Afrika ipatikanayo katika makazi ya maji ya Ziwa. Kijografia hifadhi hii inapatikana katika Ziwa Victoria Kaskazini mwa ghuba ya Emini pasha Mkoani Geita.

Hifadhi ya Rubondo ina ukubwa wa kilometa za mraba 457, ambapo kilometa za mraba 237 ni nchi kavu na 220 kilometa za mraba ni maji. Hifadhi hii ipo ndani ya ziwa Victoria ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani,  lenye kilometa za mraba 69,485, likitanguliwa na ziwa Superior la Amerika ya Kaskazini lenye ukubwa wa kilometa  za mraba 82,414.


Mwisho Watanzania wasikubali kusoma au kuhadithiwa  juu ya Hifadhi ya Taifa ya Visiwa vya Rubondo nenda na ujionee kwa macho. Tuthamini na kuzitunza Hifadhi zetu, kwa vizazi vya sasa na vya baadaye. Hifadhi inafikika kwa njia ya usafiri wa maji ya Ziwa Victoria ni takriban kilometa 165 kutoka   Sengerema kuelekea hifadhi, na kutoka Geita na Nzera kuna umbali wa kilometa 6 mpaka 7. 

No comments:

Post a Comment