TANGAZO


Thursday, August 25, 2016

MITIHANI YA TAIFA DARASA LA 4 NA KIDATO CHA 2 KUENDELEA KUFANYIKA KAMA KAWAIDA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo

Na Lilian Lundo - Maelezo
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaukumbusha Umma kuwa mitihani ya Taifa ya Darasa la 4 na Kidato cha 2 itaendelea kuwepo na mwaka huu itafanyika kama kawaida.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo ameyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam alipokuwa akikanusha taarifa za kutokuwepo kwa mitihani hiyo kwa mwaka 2016.

Napenda niukumbushe Umma kuwa mitihani hii ni muhimu sana katika ufuatiliji wa maendeleo ya wanafunzi wetu. Kwa hiyo mitihani yote miwili itaendelea kuwepo na mwaka huu itafanyika kama kawaida. Kama kuna watu wanawaambia kuwa haitafanyika wawapuuze kabisa,” alifafanua Dkt. Akwilapo.

Dkt. Akwilapo aliendelea kwa kusema kuwa, mitihani hiyo ina umuhimu mkubwa katika kupima maendeleo ya mwanafunzi kwa lengo la kufanya maendeleo ya kitaaluma. Aidha kwa wanafunzi ambao watakuwa hawajafikia viwango vya ufaulu vilivyowekwa watatakiwa kukariri darasa au kidato.

Amebainisha kuwa Baraza la Mitihani ndilo lenye jukumu la kushughulikia maandalizi ya mitihani hiyo ikiwa ni pamoja na utungaji, uchapaji, ufungaji na usafirishaji hadi ngazi ya Mkoa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) ikiwa na majukumu ya kuhakikisha kuwa uendeshaji na usahihishaji wa mitihani hiyo unafanyika kikamilifu.

No comments:

Post a Comment