TANGAZO


Thursday, August 25, 2016

DED BUNDA AMSIMAMISHA KAZI MTHAMINI

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara, Bibi. Janeth Mayanja.

Na Immaculate Makilika- MAELEZO
MKURUGENZI Mtendaji  wa Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara, Bibi. Janeth Mayanja amemsimamisha kazi mtumishi wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji kwa kosa la kujipatia fedha kinyume na taratibu za utumishi wa umma.

Akizungumza leo mjini Bunda wakati wa tukio hilo, Bi. Mayanja alisema kuwa ameamua kumsimamisha kazi  kwa muda, Bw.Eliudi Haonga ambaye ni mtumishi wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji pia ni Mthamini wa Halmashauri  hiyo ili kupisha uchunguzi  kwa kosa la kujipatia fedha kinyume na taratibu za utumishi wa umma.

“Tarehe 28 mwezi Juni mwaka huu  Bw.Eliudi Haonga alipokea  fedha kiasi cha shilingi milioni saba kutoka  kiwanda cha Olam ikiwa ni kodi ya pango kwa mwaka kodi 2015/2016, lakini mtumishi huyo  alihifadhi kwenye akaunti ya Halmashauri ya mji yaani ‘own source’ fedha kiasi cha  shilingi milioni mbili tu, na kiasi kilichobaki yaani milioni tano  alizitumia kwa masuala binafsi kinyume na taratibu za utumishi wa umma” alisema Bibi  Mayanja

Aliongeza kuwa Bw. Haonga aligushi risiti ya Halmashauri ya Mji na ambayo aliikabidhi katika  kiwanda cha Olam baada ya kupokea fedha hizo.

Alisisitiza kuwa mtumishi huyo amesimamishwa kazi kwa mujibu wa kifungu namba 38 (1) cha kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003.

Aidha, Bibi Mayanja  amewaasa watumishi wa umma wanaofanyakazi katika Halmashauri hiyo  kuwa  waadilifu kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi. Vile vile ameonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka.

No comments:

Post a Comment