TANGAZO


Friday, July 1, 2016

WANUFAIKA WA MIKOPO YA ELIMU YA JUU WATAKIWA KUIREJESHA MIKOPO WALIYOPEWA

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa

Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
30/06/2016
WANUFAIKA wa Mikopo ya Elimu ya Juu ambao tayari wapo katika ajira wametakiwa kurejesha marejesho ya mikopo waliyopewa kutokana na mfuko wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kutegemea fedha hizo kuendelea kuwakopesha wanafunzi wengine.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameyasema hayo jana Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akiwasilisha hotuba ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la kumi na moja.

“Uwezo wa Bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu kuwahudumia walengwa unajengwa na fedha zinazotengwa kila mwaka katika mipango na Bajeti pamoja na marejesho ya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika,” alisisitiza Mhe. Majaliwa.

Aliendelea  kusema kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho ya kimfumo na kisheria ili kuimarisha urejeshwaji wa mikopo. Aidha amewaagiza waajiri wote Nchini kutekeleza wajibu wao wa kuingiza makato ya marejesho wa mikopo ya wanufaika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa baada ya kuwasiliana na Bodi ya Mikopo.

Vile vile Mhe. Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu sambamba na kushughulikia changamoto mbalimbali zilizopo katika Bodi ya mikopo ili kuhakikisha utoaji wa mikopo unafanyika kwa ufanisi.

Pia Serikali inategemea kubadilisha utaratibu wa kutoa mikopo ili kuwafikia wanafunzi wote wenye uhitaji zaidi wakiwemo yatima na wenye uwezo mdogo kiuchumi bila kujali aina gani ya program wanazozisomea.



HALMASHAURI ZOTE NCHINI ZATAKIWA KUTUMIA MIFUMO YA KIELEKTRONIKI KATIKA KUKUSANYA MAPATO

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa

Na Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
01/07/2016
WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri zote Nchini kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato kuanzia Julai 01, 2016.

Mhe. Majaliwa aliyasema hayo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akihitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la kumi na moja Juni 30, 2016.
“Napenda kutumia fursa hii kuziagiza Halmashauri zote Nchini kwamba kuanzia tarehe Mosi Julai, 2016 zihakikishe zinatumia mifumo ya kieletroniki katika kukusanya mapato, katika kulipa, kuweka na kutekeleza kikamilifu mikakati madhubuti ya kuboreshha makusanyo,” alifafanua Mhe. Majaliwa

Aidha Mhe. Majaliwa amezitaka Halmashauri hizo kutoelekeza vyanzo vyote vya mapato kukusanywa na mawakala kwani vipo vyanzo ambavyo vinaweza kukusanywa kwa ufanisi na Halmashauri zenyewe bila kutegemea mawakala.

Aliendelea kusema kuwa, Halmashauri zitaelekezwa kwa waraka ni vyanzo vipi vitahitaji kutumia mawakala na vingine vitakusanywa na Halmashauri zenyewe kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Serikali.

Mhe. Majaliwa aliitaja miongozo hiyo kuwa ni pamoja na Halmashahuri aidha kwa kutumia mawakala  au Halmashauri zenyewe kuweka kwenye akaunti ya Halmashauri  fedha zote zinazokunywa kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ili kupunguza na kumaliza kabisa masuala ya (cash transactions).

Vile vile Halmashauri zikubaliane na wakala ni kiasi gani cha asilimia ya makusanyo kitalipwa kwa wakala na malipo yafanyike baada ya kukusanya na kuingizwa kwenye akaunti ya Halmashauri.

Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa sura 290, inazipa uwezo mamlaka za Serikali za Serikali za Mitaa kutoza na kukusanya kodi, ushuru na ada mbalimbali kama vyanzo vya mapato vya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Sheria hiyo pia inazipa mamlaka hizo kuteua Mawakala wa kukusanya mapato hayo kwa niaba ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu.

No comments:

Post a Comment