TANGAZO


Wednesday, May 25, 2016

WAZAZI FUATILIENI MAENDELEO YA WATOTO WENU SHULENI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako.

Na Fatma Salum- MAELEZO, Dodoma.
25/05/2016
WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao shuleni ili waweze kumudu stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu  na  kufanya vizuri kwenye mitihani yao.

Hayo yamesemwa leo bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Profesa Joyce Ndalichako wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Bi. Mariam Kisangi alilohoji kama Serikali imefanya utafiti wa kina kuhusu  wanafunzi kutojua kusoma na kuandika.

Profesa Ndalichako alisema kuwa ili watoto waweze kufanikiwa kitaaluma  wazazi na walezi wanapaswa kushirikiana na walimu na kufuatilia maendeleo ya masomo ya watoto wao mara kwa mara na kuacha tabia ya kudhani kuwa jukumu hilo ni la walimu peke yao.

“Natoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwapa ushirikiano wa kutosha walimu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.” alisema Prof. Ndalichako.
  
Pia Profesa Ndalichako alieleza kuwa  wazazi na walezi wana jukumu la kuhakikisha watoto wao wanahudhuria shuleni kila siku kwa wakati na wanafanya kazi na mazoezi yote wanayopewa na walimu wao ikiwemo kusaidia kuwaelekeza pale inapohitajika. 

Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako ufuatiliaji unaofanyika kupitia Wadhibiti Ubora wa Shule na wataalamu mbalimbali wa elimu imethibitika kuwa mwalimu ana nafasi kubwa katika kumwezesha mwanafunzi kujua kusoma, kuandika na kuhesabu lakini kuna mambo muhimu ya kuzingatia ili mwalimu huyo aweze kufanya kazi yake kwa ufanisi na kumsaidia mwanafunzi ipasavyo.

Miongoni mwa mambo hayo alibainisha kuwa ni pamoja na uwiano sahihi wa mwalimu na wanafunzi katika darasa, upatikanaji wa vitabu na vifaa na zana za kufundishia , mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia na ushirikiano mzuri kati ya mwalimu na wazazi au walezi.

“Kwa kuzingatia hayo Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuimarisha ufundishaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ikiwemo kutoa mafunzo kazini kwa walimu wa stadi hizo na imeshatoa mafunzo kwa walimu 22,697 na imeandaa na kusambaza vitabu mashuleni ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa urahisi.“Alisema Ndalichako.

Pia aliongeza kuwa Serikali inajitahidi kuhakikisha vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana kwa wakati na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara. 

Baadhi ya wazazi na walezi nchini hawana budi kubadilika na kuacha tabia ya kutofuatilia maendeleo ya watoto shuleni kwa kudhani kuwa jukumu la kuboresha elimu ni la mwalimu na Serikali kwani tabia hiyo inachangia kuzorota  kwa maendeleo ya wanafunzi na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment