TANGAZO


Wednesday, May 25, 2016

SERIKALI YAADHIMISHA SIKU YA AFRIKA KWA KUMUENZI NGULI MPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA HAYATI KALUTA AMRI ABEID KALUTA

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mh. Sofia Mjema (kulia), akiongoza msafara wa ujembe kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuzuru Kaburi la nguli mpigania Uhuru wa Tanganyika Hayati Kaluta Amri Abeid Kaluta katika kuadhimisha Siku ya Afrika leo, jijini Dar es Salaam. Katikati ni  Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bibi. Nuru Halfan Mrisho na kushoto ni Naibu Meya Bw. Salum Faisal. (Picha zote na Genofeva Matemu – Maelezo)
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Halfan Mrisho, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sofia Mjema wakiokota baadhi ya uchafu katika kaburi la nguli mpigania Uhuru wa Tanganyika, Hayati Kaluta Amri Abeid Kaluta walipozuru kaburi hilo, katika kuadhimisha siku ya Afrika leo, jijini Dar es Salaam. Wapili kushoto ni mtoto wa tano wa hayati Sheikh Kaluta Bw. Amiri Kaluta Amri Abedi na kulia ni Naibu Meya Bw. Salum Faisal. 
Mtoto wa tano wa hayati sheikh Kaluta Bw. Amiri Kaluta Amri Abedi (watatu kulia) akiongoza dua ya kumuombea baba yake hayati sheikh Kaluta Amri Abeid wakati ujembe kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ulipozuru katika kaburi la nguli huyo kuadhimisha siku ya Afrika leo Jijini Dar es Salaam. 
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sofia Mjema (kushoto mbele) akizungumza wakati ujumbe kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ulipozuru katika kaburi la nguli mpigania Uhuru wa Tanganyika Hayati Kaluta Amri Abeid Kaluta kuadhimisha siku ya Afrika leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo Bibi. Nuru Halfan Mrisho. 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Halfan Mrisho (kulia) akizungumzia siku ya Afrika alipozuru katika kaburi la nguli mpigania Uhuru wa Tanganyika Hayati Kaluta Amri Abeid Kaluta  kuadhimisha siku ya Afrika leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto mbele ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sofia Mjema. 
Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Taifa Dkt. Suleimani Sewangi (mwenye miwani) akisoma tawasifu ya hayati Sheikh Kaluta Amri Abeid  Kaluta wakati ujumbe kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ulipozuru katika kaburi la nguli huyo kuadhimisha siku ya Afrika leo Jijini Dar es Salaam. 
Bw. Kassim Amotile (mwenye miwani) akigani Shairi lililoandikwa na marehemu Mathias Mnyampala mwaka 1964 wakati wa kifo cha hayati Sheikh Kaluta Amri Abeid Kaluta na kulipa jina la Kifo cha Sheikh Abeid, Pengo kuu kwa Taifa wakati ujumbe kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ulipozuru katika kaburi la nguli huyo kuadhimisha siku ya Afrika leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sofia Mjema na wapili kulia ni Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara hiyo Bibi Nuru Halfan Mrisho

Na Genofeva Matemu – Maelezo
Tarehe: 25/05/2016
MAMLAKA ya Halmashauri ya Wilaya ya Temeke imeagizwa kuandaa siku maalumu itakayowawezesha wananchi wakiwemo wanafunzi kuzuru kaburi la nguli mpigania uhuru wa Tanganyika Hayati Kaluta Amri Abeid Kaluta na kulifanya kuwa eneo la kiutamaduni na kihistoria.

Rahi hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sophia Mjema alipoongozana na ujumbe kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuzuru kabuli la nguli huyo katika kuadhimisha siku ya Afrika leo Jijini Dar es Salaam.

“Nguli kama Hayati Abeid Kaluta ni watu wenye historia kubwa katika kupigania uhuru wa Tanganika ni vyema Uongozi wa Wilaya ya Temeke kuandaa siku maalumu na kuialika familia yake kuzuru kaburi hili na kupata historia ya Tanganyika kupitia nguli huyu” alisema Mhe. Mjema.

Aidha Mhe. Mjema ametoa rai kwa wakuu wa wilaya zote nchini kutambua mashujaa waliopigania uhuru wa Tanganyika kwa kutambua shule na mitaa ama maeneo yanayotumia majina ya mashujaa hao kwa kuwaenzi na kusambaza historia zao kwa jamii inayowazunguka.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Halfan Mrisho amesema kuwa Wizara imeamua kuzuru kaburi la Hayati Kaluta Amri Abeid kama njia ya kuenzi mchango wa shujaa huyo na kuhabarisha umma historia ya shujaa Abeid ambaye walio wengi hawamjui na hawafahamu mchango alioutoa kwa nchi  hii.

Bibi. Mrisho amesema kuwa uwepo wa kaburi la Hayati Kaluta Amri Abeid ni fursa ya kipekee ya kutangaza utalii wa kiutamaduni na eneo la kihistoria katika Wilaya ya Temeke.


Hayati Sheikh Amri Abeid Kaluta alizaliwa mwaka 1924 Mkoani Kigoma na kufariki dunia mwaka 1964 huko Boni nchini Ujerumani. Ametoa mchango mkubwa katika Taifa kwa kuwa mwanaharakati mpigania uhuru kwa kutumia silaha ya mashairi, ni mkuzaji na muenezaji wa Utamaduni, utanzu wa fasihi na alikuwa Sheikh Mkuu wa kidini dhehebu la Ahmadiyya.

No comments:

Post a Comment