TANGAZO


Tuesday, July 28, 2015

Rais Dk. Shein aitaka Sekta binafsi kujenga utamaduni wa kutoa ruzuku za tafiti kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua rasmi Jengo Jipya la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) Ofisi ya Zanzibar liliopo ndani ya majengo ya zamani ya ilichokuwa kiwanda cha Sigara Maruhubi Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif wa pili kutoka Kushoto akipata maelezo kutoka kwa Wataalamu  wa Chuo cha Utafiti Kizimbani  wakiongozwa na Said Suleiman Bakari jinsi zao la viazi vitamu linavyoweza kutumiwa vyema katika utengenezaji wa Juisi. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Majini Magharibi Mh. Abullah Mwinyi.
Watafiti na wawakilishi wa Vikundi vya wajasiri amali waliopata ufadhili kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia wakimpatia maelezo Balozi Seif wakati akiangalia maonyesha mara baada ya kulifungua Jengo la Tume hiyo.
Baadhi ya Wataalamu na wajasiri amali kutoka vikundi tofauti Nchini wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo Jipya la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Balozi Seif akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Jengo la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia hpo Maruhubi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziI Dr. Ali Mohammed Shein.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) mara baada ya uzinduzi wa jengo la Tume hiyo hapo Maruhubi. Kulia ya Balozi Seif ni Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Ali Juma Shamuhuna, Mkurugenzi Mkuu wa Costech Dr. Hassan Mshimba, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Dr. Idriss Rai.

Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Kanal MstaafuJoseph Simba Kalia, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Abdullah Mwinyi pamoja na Naibu Katibu Mkuu Osifi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)

Na Othman  Khamis Ame
Ofisi  ya  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
28/7/2015.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein amesema wakati umefika kwa sekta binafsi kujenga Utamaduni wa kutoa ruzuku za tafiti kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ili ijipatie nguvu za ziada za uwezeshaji wa kuendesha shughuli zake za utafiti kama nchi nyengine Duniani zilizofanikiwa kwa kufuata mfumo huo.

Alisema kufanya utafiti kunahitaji nguvu kubwa ya fedha kiasi kwamba Serikali pekee haiwezi kumudu kugharamia bila ya kushirikisha taasisi mbali mbali za sekta binafsi za ndani na nje ya nchi.

Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa ufunguzi wa Jengo la Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia { COSTECH } liliopo Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania imeonyesha mwanga wa kusaidia jamii kwenye tafiti za kina za Kimaendeleo zitakazomkomboa Mtanzania kutoka katika dimbwi la umaskini na kuelekea kwenye maendeleo ya kweli.

Alieleza kwamba Costech imekuwa na jitihada katika uendelezaji wa rasilmali watu ya wataalamu waliopo Zanzibar inayowagharamiwa  kimasomo kwa shahada yao ya uzamivu na uzamili katika kiwango cha Master na Udokta kwenye vyuo mbali mbali ndani na Nje ya Nchi ambao kwa sasa wapo 22 kutoka Zanzibar.

“ Tume ya Taifa ya Sayansi na Tekonolojia pia tunaishukuru kwa kuratibu na kugharamia tafiti tofauti zinazosimamiwa na vyuo mbali mbali vya Zanzibar kama SUZA, IMS, ZIFFA na Taasisi ya Utafiti Kizimbani “. Alisema Dr. Shein.

Alifahamisha kwamba Costech kwa kushirikiana na Tume ya Mipango Zanzibar pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar tayari imeshaanda agenda ya utafiti ya Zanzibar ili Serikali iweze kuitumia katika maamuzi ya vipaumbele vya Tafiti kwa maendeleo ya jumla ya Taifa.

Dr. Shein alisema hilo ni jambo zuri katika muelekeo wa kunyanua ustawi wa Umma na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake itakuwa tayari kutumia matokeo  ya tafiti zinazofanywa na Wasomi wa hapa Nchini kupitia Tume hiyo.

Hata hivyo Dr. Shein aliitanabahisha Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kwamba yale matokeo ya utafiti yanayostahili kuwafika moja kwa moja Wananchi yatolewe ili kuwapa fursa wananchi hao kuelewa kinachoendelea kwenye maisha yao ya kila siku.

Rais wa Zanzibar ameipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa uamuzi wake wa busara wa kuanzisha Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia.

Alisema uamuzi huu unadhihirisha wazi jinsi Tume hiyo Chini ya Wizara yake ilivyopania kukuza maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa pande zote mbili za Muungano ambapo Taasisi hii ndio msimamizi na mshauri Mkuu wa Serikali kwa masuala yote yanayohusu sayansi, ugunduzi na Teknolojia kwa maendeleo ya Taifa.

Dr. Shein alielezea matumaini yake  binafsi na yale ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba  uwepo wa Ofisi ya Tume hiyo kutaongeza kasi kwa Wasomi wa hapa Nchini kuendelea kufanya tafiti mbali mbali na kuongeza kasi ya shughuli za ubunifu katika nyanja tofauti.

Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Taasisi nyengine za Serikali ya Muungano wa Tanzania na zile Binafsi za Tanzania Bara mbazo hazijafungua Ofisi zao hapa Zanzibar kufanya hivyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kuwapatia maeneo ya kujenga Ofisi hizo kwa lengo la kuwarahisishia Wananchi kupata huduma za karibu.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH  Dr. Hassan Mshimba alisema ujenzi wa Ofisi ya Tume hiyo hapa Zanzibar  ni kutekekeza ahadi iliyotoa Uongozi wa Taasisi hiyo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mwaka 2012.

Dr. Hassan Mshimba alisema kwamba Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kwa kuona umuhimu wa zao la Mwani kwa Serikali ya Mapinduzi ilitoa Vihori 100 vya kubebea mwani kwa lengo la kuwawezesha wakulima wa zao hilo Unguja na Pemba kukuza Kilimo hich ikiwa ni miongozi mwa miradi sita inayotekelezwa na Tume hiyo kwa Upande wa Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Costech alisisitiza kwamba katika azma ya kukuza ajira Nchini Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia imekusudia kuungana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha vitengo vya Utafiti Zanzibar kama alivyosisitiza Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein siku ya Utafiti Tarehe 12 Disemba mwaka 2014.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Kanal Mstaafu Joseph Simba Kalia ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa ukarimu wake wa kutoa Jengo kwa ajili ya Ofisi za Tume hiyo.

Kanal Mstaafu Simba Kalia alisema kitendo hicho kilichofanywa na  SMZ ni uthibitisho wa kuthamini umuhimu wa fani ya Utafiti ambayo ndio chachu ya maendeleo ya jambo lolote lile hapa Ulimwenguni.

Ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ilizinduliwa  rasmi mnamo Tarehe 11 Juni Mwaka 2012 katika Majengo ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyopo Tunguu Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na kuanza kutoa huduma zake hapa Zanzibar.

Ofisi hiyo ya  Costech iliyofanyiwa matengenezo kwa kipindi cha miezi 12 imegharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni 185,000,000/-  ikiwa na vyumba sita vya Ofisi pamoja na ukumbi wa Mikutano ipo kwenye  majengo ya zamani ya ilichokuwa Kiwanda cha utengezezaji Sigara baridi katika eneo la Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment